Kamati ya Utendaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Desemba 19 mwaka huu)
jijini Dar es Salaam, imezingatia upungufu uliopo katika utekelezaji wa
matumizi ya tiketi za elektroniki.
Hivyo, Kamati hiyo imeiagiza
Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na benki ya CRDB inayoendesha mfumo huo
wa matumizi ya tiketi za elektroniki kuhusu upungufu huo na kuhakikisha
unafanyiwa kazi.
MAREKEBISHO YA KATIBA YA TFF
Kamati ya Utendaji ya TFF imerejea
mazungumzo kati yake na ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) uliokuwa nchini ukiongozwa na Meneja wa Vyama Wanachama wa
FIFA, James Johnson.
Mazungumzo hayo kuhusu Katiba ya TFF yalifanyika Desemba 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kamati ya Utendaji inasubiri
rasimu ya Katiba hiyo kutoka FIFA ili iweze kufanya utaratibu wa
kuwaarifu wanachama wake juu ya maudhui ya rasimu hiyo.
Shughuli ya FIFA kurekebisha
katiba za nchi wanachama wake inaendelea duniani kote, na kwa Afrika
kazi hiyo imekamilika katika nchi za Namibia, Zimbabwe na Malawi.
USHIRIKIANO KATI YA TFF NA SAFA
Kamati ya Utendaji imepitia na
kupitisha makubaliano ya ushirikiano kati ya TFF na Chama cha Mpira wa
Miguu Afrika Kusini (SAFA).
Makubaliano hayo ni ushirikiano
katika nyanja za mpira wa miguu wa vijana, maendeleo ya waamuzi, ufundi,
menejimenti ya matukio (event management) na utafutaji udhamini
(sponsorship).
KANUNI ZA LESENI ZA KLABU (CLUB LICENSING REGULATIONS)
Kamati ya Utendaji imejadili
rasimu ya Kanuni za Leseni za Klabu (Club Licensing Regulations), na
kuagiza Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ifanye marekebisho ya
mwisho, kabla ya kanuni hizo kusainiwa na kuanza kutumika.
UANZISHAJI MFUKO WA MAENDELEO YA MPIRA WA MIGUU (FDF)
Kamati ya Utendaji imepokea
taarifa ya maendeleo ya mchakato wa uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya
Mpira wa Miguu (Football Development Fund- FDF).
Imeipongeza Kamati ya Mfuko huo
inayoongozwa na Rais wa zamani wa TFF, Leodegar Tenga, na kuitaka fanye
jitihada za kukamilisha rasimu ya kanuni za uendeshaji mfuko huo.
Mbali ya Tenga, wajumbe wengine wa
mfuko huo ni Ayoub Chamshama, Ephraim Mafuru, Frederick Mwakalebela,
Tarimba Abbas na Zarina Madabida. Sekretarieti ya mfuko huo inaundwa na
Henry Tandau ambaye ni Katibu, Wakili Emmanuel Muga na Boniface Wambura.
FDF ambao ni mfuko utakaokuwa
unajitegemea utakuwa unashughulika na maendeleo ya mpira wa miguu kwa
vijana, na nyanja nyingine za maendeleo kwa mchezo huo.
MKUTANO MKUU KUFANYIKA SINGIDA MACHI 14
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepanga Mkutano Mkuu wa Kawaida wa
mwaka ufanyike Machi 14 na 15 mwakani mjini Singida.
MGOGORO NDANI YA ZFA
Kamati ya Utendaji imepokea kwa masikitiko taarifa za masuala ya mpira wa miguu Zanzibar kupelekwa mahakamani.
Kwa mujibu wa Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kitendo hicho ni kinyume cha taratibu
za uendeshaji mpira wa miguu ambazo zinakataza masuala ya mchezo huo
kupelekwa katika mahakama za kawaida.
Kamati ya Utendaji inatoa rai kwa
pande zote mbili zinazohusika na mgogoro huo kukaa kwenye meza ya
mazungumzo ili kumaliza tofauti zao. Kamati ya Utendaji imejitolea
kutuma ujumbe wake Zanzibar ili ukutane na pande zinazohusika katika
mgogoro huo.Ni muhimu usuluhisho upatikane haraka ili tuweze kujua hatma
ya washiriki wetu kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment