WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imeamua kutafuta soko la utalii
kutoka nchi za Ghuba na Mashariki ya Kati ili kuongeza idadi ya watalii
nchini na kukuza pato la Taifa kupitia sekta hiyo.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Desemba 17, 2014)
wakati akizungmuza an waandishi wa habari mara baada ya kufungua
Kongamano la siku mbili la Utalii na Uwekezaji lilionza leo kwenye
hoteli ya Le Meridien, jijini Dubai, Falme za Kiarabu.
“Tunao mkakati wa kukuza utalii
nchini lakini wengi wameskuwa wakitoka Ulaya na Marekani. Eneo ambalo
tumeona tuwekeze kwa nguvu kwa maana ya kuongeza idaidi ya watalii ni
hili la nchi za ghuba na Mashariki ya Kati,” alisema.
Waziri Mkuu alisema kimahusiano
Tanzania iko karibu na nchi hizi za ghuba lakini pia wanao uwezo wa
kifedha wa kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ya utalii. “Amani ya nchi
yetu ni kivutio kingine kikubwa cha uwekezaji, sisi tuko tayari
kuwasaidia wafike huko tunakotaka,” alisema.
Alitoa wito kwa makampuni
yanayotaka kuwekeza nchini yaangalie fursa zilizopo kwenye ujenzi wa
hoteli za kawaida, hoteli za mahema (tented camps) na hoteli zenye kutoa
huduma za vyakula (special cuisine restaurant).
Hata hivyo, aliwataka wawekezaji
watakaokuja wafanye juhudi ya kushirikiana na Watanzania wazawa ili nao
wajione ni sehemu ya uwekezaji huo.
Mapema, akifungua mkutano huo,
Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka mitano, Tanzania imeweza
kuongeza idaidi ya watalii kutoka 714,367 mwaka 2009 hadi kufikia
watalii 1,095,884 kwa mwaka 2013.
“Kiwango cha mapato ya watalii hao
kiliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.2 hadi kufikia dola za
Marekani bilioni 1.8 katika kipindi hicho hicho cha miaka mitano,”
alisema na kuongeza kuwa sekta hiyo inaajiri watu zaidi ya 400,000
kuchangia asilimia 17 kwenye pato la Taifa.
Naye Waziri wa Maliasili na
Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu akizungumza na washiriki wa kongamano hilo
kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu alisema Tanzania ni nchi ya pili
duniani kwa kuhifadhi rasilmali zake na kuzitumia kwa utalii. “Nchi
inayoongoza duniani ni Brazil,” alisema.
Akiainisha fursa za uwekezaji
zilizopo Tanzania, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii nchini
(TTB), Bi. Devothe Mdachi alisema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji
kupitia sekta ya utalii zikiwemo uendelezaji wa fukwe, michezo ya
majini na utalii wa mikutano (conference tourism).
“Kwenye kumbi za mikutano,
Tanzania inahitaji kumbi kubwa zenye uwezo wa kuchukua watu kati ya
5,000 na 10,000 na hasa kwenye miji mikubwa kama Arusha, Dar es Salaam
na Mwanza,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha
Uwekezaji nchini (TIC), Bibi Julieth Kairuki aliwaeleza washiriki wa
kongamano hilo kwamba utalii una fursa kubwa ya uwekezaji kama ilivyo
kwenye sekta nyingine za madini na uchumbaji gesi.
“Uwekezaji hivi sasa umepanuka, na
soko la utalii nchini Tanzania ni fursa kubwa sana ya kuwekeza.
Tunawasihi watu wenye mitaji mikubwa waangalie fursa hiyo na
kuichangamkia kama njia mojawapo ya kuwekeza nchini Tanzania,” alisema.
No comments:
Post a Comment