Mechi ya Mtani Jembe nchini
Tanzania, inayozikutanisha timu mbili za jijini Dar es Salaam zenye
ushindani wa jadi, za Simba na Yanga imegeuka uwanja wa machinjio kwa
makocha wa Yanga kwa mara ya pili mfululizo.
Mechi kama hiyo
ilipofanyika mwaka jana, 2013, Yanga ilifungwa magoli 3-1 na kusababisha
aliyekuwa kocha wake Ernie Brandts kutimuliwa pamoja na benchi lake la
ufundi. Mwaka huu ni zamu ya kocha Marcio Maximo kufungashiwa virago
vyake baada ya kunyukwa mabao 2-0 katika mechi ya Mtani Jembe
iliyofanyika Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam, na huu ukiwa ni mchezo wa nane wa ushindani baada ya michezo
saba tu ya ligi kuu ya Vodacom ya nchi hiyo.
KOCHA Maximo ambaye
alipokelewa kwa vifijo na nderemo na mashabiki na wanachama wa Yanga
mwezi Juni mwaka huu baada ya kutangazwa kuwa kocha mpya wa timu yao,
amewaaga rasmi wachezaji wa timu hiyo kwenye mazoezi uwanja wa Sekondari
ya Loyola ya jijini Dar es Salaam.
Mazoezi hayo ya Jumanne
asubuhi yaligeuka simanzi baada ya Maximo kuwakusanya wachezaji wake na
kuwambia kuwa kuanzia hiyo jana hakuwa kocha wa timu hiyo tena na
kuwatakia maisha mema ndani ya klabu hiyo ya Jangwani.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti wachezaji wa klabu hiyo walielezea kutoridhishwa na
uamuzi wa uongozi wa klabu hiyo kumuacha kocha wao na mshambuliaji
Hamis Kiiza kutoka Uganda.
Mmoja wa wachezaji hao alisema "Ni kweli kocha ametuaga asubuhi daa!
ndio hivyo tumesikitika lakini hatuna jinsi."
Naye
mchezaji mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema "Inaumiza
sana jana (juzi) tumefanya nae mazoezi vizuri kabisa tena amechangamka
kama kawaida kumbe nyuma kuna mambo yanaendelea, leo asubuhi tumeenda
mazoezi kama kawaida tukijua tunafanya mazoezi matokeo yake anasema
acheni kila kitu kaeni hapo nataka kuzungumza na nyinyi".
Mchezaji
mwingine wa timu hiyo alisema "Hakuna mchezaji kwa kweli aliyependezwa
na kitendo cha uongozi, yaani kwenye mazoezi asubuhi ilikuwa kama msiba,
'mood' ya kufanya mazoezi iilisha kabisa, yaani hakuna aliyekuwa na
hamu ya kuendelea na mazoezi.
"Tumefanya kidogo mazoezi
tukaondoka, ukiangalia ni sawa tumefungwa cha muhimu ilikuwa ni kukaa
chini na kuzungumza na kuangalia cha kufanya, kama kuna mapungufu basi
yafanyiwe kazi, mimi sijaona haja ya kumfukuza kocha hasa kipindi kama
hichi."
Meneja wa timu hiyo Hafidhi Saleh alikiri Maximo kuwaaga
wachezaji kabla ya mazoezi ya timu hiyo kwanza akiwapa moyo wajitume kwa
kuwa ni wachezaji wazuri na timu ni nzuri na kuwataka kuongeza bidii
ili wafike mbali.
"Kwa kweli inasikitisha hakuna mchezaji wala mtu
aliyefurahia, kama yupo labda kimoyomoyo ila dah imetuumiza, ni mazoea
cha muhimu tugange yajayo hayo mengine tuwaachie viongozi."alisema Saleh
Mchezo
wa Mtani Jembe ambao ni wa kujifurahisha na kuongeza utani kati ya timu
hizo, umegeuka kuwa kipimo cha ubora wa kocha hata kama kocha huyo
anafanya vizuri katika michezo ya ligi kuu. Hadi wakati anafukuzwa,
kocha wa Yanga Mbrazil Marcio Maximo, timu yake inashika nafasi ya pili
baada ya Mtibwa inayoongoza katika msimamo wa ligi hiyo kutokana na
michezo saba tu iliyochezwa.
Baadhi ya mashabiki wameunga mkono
uamuzi wa kumtimua Maximo wakisema timu haikuwa na uwezo wa kupambana na
timu pinzani, huku wengine wakipinga uamuzi huo kuwa haukustahili
kuhukumu uwezo wa kocha huyo katika mchezo mmoja wa kirafiki na kusahau
nafasi inayoshikiliwa na timu katika msimamo wa ligi kuu
No comments:
Post a Comment