Na Anna Nkinda – Maelezo, aliyekuwa Lindi
Wakazi wa mkoa wa Lindi
wametakiwa kuunganisha nguvu zao na kujitolea kuchangia madawati ili
kuboresha elimu ya watoto ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu na
mazingira bora ya kufundishia na kujifunza.
Rai hiyo imetolewa jana na Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete wakati wa hafla fupi ya kukabidhi sampuli za
madawati katika shule za msingi kwa ajili ya wanafunzi wa madarasa ya
awali kwa uongozi wa Manispaa ya Lindi iliyofanyika katika shule ya
Msingi Rahaleo.
Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti
wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema mkoa huo umekuwa
nyuma kielimu kwa muda mrefu hivyo basi ni jukumu la jamii kushirikiana
kwa pamoja na kuwekeza katika elimu ili watoto wapate elimu bora
ambayo itawasaidia katika maisha yao.
“Wazazi, walezi na wananchi
tunapaswa kuona aibu na kutovumilia kuona wanafunzi wanakaa chini. Hii
siyo aibu ya Serikali bali ni aibu yetu sisi wazazi na walezi na
viongozi wa Kata na Wilaya”.
Tatizo la madawati liko ndani ya
uwezo wetu hatuwezi kusubiri Serikali kuu hadi watakavyokuwa tayari.
Tunachangia maharusi na shughuli nyingine lakini tunashindwa kuchangia
kwenye elimu, inasikiisha”, alisema.
Mama Kikwete pia aliwataka
viongozi wa mkoa huo kuweka suala la madawati katika vipaumbele vyao
kwa muda maalum kwani ukimuandaa mtoto katika umri mdogo na kumjengea
mazingira mazuri ya kusoma ikiwa ni pamoja na kukaa katika madawati
atapenda shule na hata mwandiko wake utakuwa mzuri.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya
Lindi Dkt. Nassor Hamid aliwataka walimu wa shule za awali kufanya
jitihada na kuhakikisha watoto wanajua kusoma na kuandika kabla
hawajaingia darasa la kwanza kwani ni aibu kuona mtoto anaingia darasa
la kwanza hajui kusoma wala kuandika.
“Shule za awali ni mahali ambapo
vipaji vya watoto vinatambuliwa ni muhimu kwa walimu wakati wanaandika
ripoti za wanafunzi kwa wazazi wakaandika na vipaji walivyovitambua
kutoka kwa watoto hao hii itasaidia kuviendeleza”, alisema Dkt. Hamid.
Akisoma taarifa ya elimu ya
manispaa ya Lindi Hassan Yusufu ambaye ni mwalimu Mkuu wa shule ya
Msingi Rahaleo alisema wanafunzi wa madarasa ya awali wanatumia vyumba
vya madarasa ya shule za msingi isipokuwa shule ya msingi Mtanda ambayo
inavyumba viwili vya madarasa ya awali.
Mwalimu Yusufu alisema, “Wanafunzi
wa elimu ya awali kwa kiasi kikubwa wanatumia thamani za shule ya
Msingi. Shule chache zina madawati ya wanafunzi wa awali na baadhi ya
shule zilipata msaada wa thamani kutoka kwako Mama Kikwete tunashukuru
sana. Msaada huu umekuwa na manufaa sana kwetu katika kujenga misingi
imara ya wanafunzi”.
Mwalimu huyo alisema mahitaji ya
madawati katika manispaa hiyo ni 752 kwa shule za awali yaliyopo ni 448
na kwa shule za msingi ni madawati 3,994 yaliyopo ni 3,537 hivyo kuwa
na upungufu wa madawati 304 kwa shule za msingi na 699 kwa shule za
awali.
Halmashauri ya Manispaa ya Lindi
ina jumla ya shule za msingi 32 kati ya hizo za Serikali ni 31 ambazo
zote zina madarasa ya awali na moja ya binafsiKatika madarasa ya awali
kuna jumla ya wanafunzi 1803 kati ya hao wavulana 920 na wasichana 883.
No comments:
Post a Comment