Mke wa Rais Mama Salma Kikwete |
Na: Anna Nkinda – Maelezo
18/12/2014 Vijana wametakiwa
kujiunga na vikundi vya kuweka akiba na kukopa ili kuchangia mawazo yao
na ubunifu na wakati huo huo wanajitengenezea mazingira ya kujiajiri
kwani wengi wao wana elimu na ujuzi walioupata masomoni lakini
wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira.
Rai hiyo imetolewa leo na Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete wakati akizindua Umoja wa Vikundi vya kuweka
Akiba vilivyopo chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wilaya
ya Kinondoni (UWAMAKI) katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha
Usafirishaji jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA alisema kupitia vikundi hivyo vijana
wanaweza kupata mitaji midogomidogo pamoja na mafunzo ya kuwawezesha
kuanzisha biashara na kujiajiri. Kwani mfumo huo wa vikundi na mafunzo
ni moja ya njia za kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na hivyo
kupunguza tatizo la ajira.
Kwa upande wa wanachama wa UWAMAKI
aliwasisitiza kutoridhika na mafanikio waliyoyapata bali waendelee
kutafuta njia za kupiga hatua hususani kupata utaalamu wa kuboresha
bidhaa zao , kutafuta masoko zaidi na kufanya ubunifu wa kuweza kuvumbua
bidhaa na biashara nyingine tofauti ili kuepukana na ushindani wa soko.
“Mnapokuwa na bidhaa zinazofanana
mtakuwa katika mazingira ya kushindania soko jambo ambalo litapunguza
kiasi cha mauzo ambayo ndiyo pato lenu wajasiriamali. Jitihada ifanywe
ili kuweza kutafuta watalaam ambao watawapa mafunzo ya kukuza biashara”,
alisema Mama Kikwete.
Akisoma risala ya vikundi hivyo
Katibu wa UWAMAKI , Mwajuma Waziri aliishukuru Taasisi ya WAMA kwa
kuwawezesha kuwa na vikundi na kupata mafunzo ya kuweka akiba, elimu ya
kibenki, usindikaji wa vyakula na huduma ya bima ya afya.
Waziri alisema, “Kutokana na
mafunzo hayo tunaweza kuanzisha miradi mbalimbali kama vile kutengeneza
sabuni za maji za kufulia, sabuni za kuoshea vyombo na kusafishia
tairizi, siagi ya karanga na batiki na hatimaye tumeweza kufungua
akaunti yetu ya Umoja katika benki ya wanawake (TWB)”.
Katibu huyo alisema walianza na
kikundi kimoja kwa kujiwekea hisa moja kwa thamani ya shilingi 1000 pia
waliweza kukopesha kiasi cha shilingi 6,300,000 mpaka mwisho wa mwaka
walivuna shilingi 12,750,000.
“Hadi sasa tunavikundi 11 vyenye
wanachama 274 kati ya hao wanaume ni wanane katika vikundi hivi
tumeweza kukopesha kiasi cha shilingi 47,500,000/= na kufikia mavuno ya
shilingi 79,739,000 kwa mwaka”, alisema.
Alimalizia kwa kusema lengo la
kuunda umoja huo ni kushirikiana katika matatizo ya kijamii, kuunda
SACCOS na kutafuta masoko ya bidhaa zao.
Taasisi ya WAMA inasimamia mradi
wa kuwawezesha wanawake kwa kuwapa mafunzo kupitia vikundi katika mikoa
ya Dar es Salaam Lindi na Pwani hadi kufikia Septemba mwaka huu jumla
ya watu 18,000 wamefikiwa kwa kupitia vikundi 688 vilivyoundwa na tayari
shilingi milioni 227 zimekusanywa na kukopeshwa.
No comments:
Post a Comment