Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Maandalizi ya Tamasha
la Krismasi inatarajia kusherehekea Sikukuu ya Krismasi kwa kugawa
vyakula na mahitaji mengine muhimu kwa baadhi ya vituo vya kulelea
yatima vya jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mjumbe wa Kamati
ya Maandalizi ya tamasha hilo, Jimmy Rwehumbiza hafla hiyo ya
makabidhiano hayo inatarajia kufanyika Desemba 20 kwenye ofisi za
Kampuni ya Msama Promotions zilizoko Kinondoni Block 41.
Rwehumbiza alisema wamefikiria
kukabidhi zawadi hizo ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo ambayo imejikita
kusaidia jamii zenye uhitaji maalum kama yatima, walemavu na wajane.
“Tumeonelea kabla ya tamasha
kufikisha mchango wetu kwa jamii, kwani sisi kama wadau wengine
tunahitajika kusaidia kupitia kidogo tunachopata,” alisema Rwehumbiza.
Katika hatua nyingine,
Mkurugenzi wa Msama Promotions aliahidi kukisaidia shilingi milioni moja
kituo cha kulelea yatima na shule ya awali ya TUVUCHIDO kilichopo
Temeke kwa Maganga ikiwa ni msadaa wa vifaa mbalimbali vitakavyosaidia
elimu kwa walengwa wa Wilayani humo.
Akizungumza katika mahafali ya
kuwaaga baadhi ya wanafunzi wanaotarajia kuanza darasa la kwanza
mwakani, hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania
na Zambia (TAZARA), Meneja Utawala wa Kampuni ya Msama Promotions,
Mussiba Essaba aliyemwakilisha Msama alisema kampuni yao ni mojawapo ya
kampuni zinazoguswa na wenye uhitaji maalum kama Yatima, walemavu na
wajane.
Essaba alisema hawaishii hapo,
wataendelea kuwa karibu na kituo hicho katika matukio mbalimbali hasa
katika kipindi cha sikukuu ya Krismasi.
Aidha hafla hiyo ilikuwa na
lengo la harambee ya kukusanya shilingi milioni 3.5 ambazo zitasaidia
kituo hicho kwa vifaa kama madaftari, kalamu, kompyuta, mashine ya
fotokopi na vinginevyo.
Naye kiongozi wa kanisa la
Lighthouse Chapel International kupitia mwakilishi wake, Coletha Mzena
liliahidi shilingi milioni moja ambako alikabidhi hundi ya shilingi
300,000.
No comments:
Post a Comment