MUIMBAJI wa nyimbo za injili na
mchungaji kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
na mwenye makazi yake nchini Kenya Solomon Mukubwa amepania kufanya shoo
ya nguvu katika Tamasha la Krismasi.
Ameeleza kuwa katika suala la
kumsifu Mungu daima huwa hafanyi utani hivyo siku hiyo atahakikisha kila
mmoja atakayefika kuondoka na baraka zake.
Solomon anasema kuwa kipaji
chake cha uimbaji amepewa na Mungu ingawa ameweza kuongeza jitihada ili
kuweza kufanikisha kipawa hicho.
Anaeleza kuwa pamoja na
kuonekana kuwa muimbaji mkubwa lakini nyimbo zake zimetokana na waimbaji
wa injili waliopo Tanzania kwani wana nafasi ya kwanza katika soko la
muziki huo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Afrika kwa ujumla.
Solomon mwenye asili ya DRC
anayetokea Goma Mashariki mwa mji huo ambapo aliweza kulelewa katika
familia iliyokuwa ikifuata mafundisho ya Mungu ingawa baba yake alikuwa
na wake wawili.
Anasema kuwa aliondoka nchini
Congo na kuachana na wazazi wake mwaka 2003 ambapo alielekea nchini
Uganda na kukaa kwa miaka mitatu na nusu ndipo alipokutana na marehemu
Angela Chibalonza aliyemuwezesha na kumpokea Nairobi nchini Kenya.
Mwimbaji huyo mwenye ndoto
nyingi ikiwemo ya kutaka kufungua kituo cha watoto yatima nchini
Tanzania anasema kuwa anaipenda nchi hii kiasi cha kuwa tayari kutoa
msaada kwa wahitaji mara kwa mara.
“Watanzania hawana mioyo ya
kinafiki ni wakarimu, wacheshi na wenye upendo ndio sababu mimi napenda
kuwa Tanzania na kutoa misada ikiwemo kuweka kituo cha kulea watoto
yatima” anasema Solomon.
Solomon Mukubwa anaelezea
alipopata ulemavu wa mkono anasema akiwa na miaka 12, alipata matatizo
ya uvimbe wa ajabu katika mkono wake wa kushoto.
“Uvimbe huo ulikuwa wa ajabu sana na hakuna aliyefahamu chanzo kilikuwa ni nini? Niliugua kwa muda wa miaka mitatu”.
Muimbaji huyo anasema wazazi
wake walihangaika kumpeleka kwa wataalam wa hospitali mbalimbali na hata
kwa waganga wa kienyeji bila mafanikio na anasema kuwa baada ya muda
huo kupita ilianzishwa hospitali moja na Wazungu karibu na nyumbani
kwao, na ndipo wataalam wa hapo waliposhindwa na kushauri akatwe mkono
kwa lengo la kunusuru uhai wake.
“Mkono wangu ulivimba sana na
baadae ukaoza hiyo ndio sababu ya kukatwa mkono wangu, unajua shetani ni
mjinga sana alinitesa kwa miaka mitatu ndiyo sababu ya kuimba wimbo wa
Mungu mwenye nguvu,” anasema.
No comments:
Post a Comment