………………………………………………………………………………………………………
Na Eleuteri Mangi-Arusha
Tanzania imepitisha Azimio
linalohusu Kinga ya Jamii lenye msingi imara wa kusimamia masuala hayo
nchini na Afrika kwa ujumla ili kuwa na maendeleo halisi kwa watu wake.
Azimio hilo limepitishwa na
kusainiwa na Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum kwa niaba ya Serikali
jijini Arusha wakati wa kufunga kongamano la kimataifa la siku tatu
kuhusu Kinga ya Jamii ambalo lilishirikisha wajumbe kutoka nchi
mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika.
Akitoa hotuba ya kufunga
kongamano hilo Waziri Saada alisema kuwa maazimio yaliyofikiwa katika
kongamano hilo yametoa mwelekeo na msingi wa kuimarisha kinga ya jamii
kwa wananchi.
“Nafurahi kusema kongamano hili
limekuwa hatua muhimu katika kutekeleza masuala ya kinga ya jamii kwa
nchi zote washiriki wa kongamano hili na Afrika kwa ujumla” alisema
Waziri Saada.
Waziri Saada alisema kuwa
maazimio yaliyofikiwa wakati wa kongamano hilo jijini Arusha yanalenga
kutumia mbinu mablimbali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuboresha
huduma za jamii kwa wananchi ikiwemo elimu bora, afya, upatikanaji wa
maji safi na salama.
Kutokana na malengo hayo,
Serikali ya Tanzania iko mstari wa mbele katika kuwekeza na kusimamia
masuala ya kinga ya jamii kwa kuwa na bajeti endelevu ili kufikia
malengo yaliyokusudiwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa
wanchi wake.
Akisoma Azimio hilo la Kinga ya
Jamii, Katibu Mkuu Wazara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile alisema kuwa
historia imejirudia ambapo yapata miaka 47 (1967-2014) iliyopita
Tanzania ilipitisha Azimio la Arusha lililolenga kupambana na maadui
watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini ambao Baba wa Taifa Mwl.
Julius Kmbarage Nyerere aliwaita ni maadui wa taifa.
Maazimio mengine yaliyofikiwa
katika kongamano hilo ni kupunguza umaskini na kukuza mitaji ya
rasilimali watu ambapo Tanzania Bara inalenga ifikapo mwaka 2025
iweimepunguza tatizo la umaskini kwa watu wake wakati Tanzania na kwa
upande wa Zanzibar inalenga kufikia hatua hiyo mwaka 2020.
Maazimio mengine ni kuwa utawala
bora ambapo Tanzania imesisitiza kuendelea kuimarisha nguvu na sauti ya
wananchi katika masuala ya kidemokrasia nchini na kutoa na kusimamia
haki za watoto, wanawake na wanaume kwa kupinga ukatili wa kijinsia,
ndoa za utotoni, mimba za utotoni pamoja na uvamizi na mauaji ya watu
wenye ulemavu wa ngozi na mauaji ya wazee.
Kwa upande wake Muwakilishi wa
UNICEF nchini Dkt. Jama Gulaid akitoa neno la shukrani aliisifu Tanzania
kwa kuanza mapema kusimamia masuala ya kinga ya jamii ikiwemo mifuko ya
hifadhi ya jamii na misaada inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF) kupitia mpango wake wa kunusuru kaya maskini zilizo katika
mazingira hatarishi.
Aidha, Dkt. Gulaid aliipongeza
Tanzania kwa kuwa na wimbo wa taifa unaozungumzia watu akiwataja kuwa
ni wanawake, wanaume na watoto pamoja na bara la Afrika na watu wake
licha ya kuwa na vivutio vizuri vya mlima Kilimanjaro, hifadhi ya
Serengeti na visiwa vya karafuu.
“Wimbo huu wa Tanzania tofauti
na nyimbo za nchi nyingine ambazo wao wanazungumzia askari, watumwa,
watawala wakiwemo Malkia na Wafalme”alisema Dkt. Gulaid.
Dkt. Gulaid aliwahakikishia
wajumbe wa kongamano hilo kuwa wote wapo salama na wapo kwenye mpango wa
kinga ya jamii kwa kuwa wametambuliwa na kubarikiwa na wimbo wa taifa
wa Tanzania ambapo wajumbe waliimba wimbo huo na kuhitimisha kongamano
hilo.
Kongamano hilo liliandaliwa na
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha, Idara ya Kuondo Umaskini
kwa kushirikiana na UNICEF, ILO, UNAIDS na EPRI ambapo washiriki wa
konngamano hilo wanatoka katika nchi za Kenya, Uganda, Bangladesh,
Afghanistan, Msumbiji, Lesotho, Malawi, Afika Kusini, Ghana, Ethiopia,
Zambia, Zimbabwe na mwenyeji Tanzania.
No comments:
Post a Comment