Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Hawa Ghasia
akiwaeleza waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam kuhusu mafanikio
ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika jana kote nchini ambapo
umefanikiwa kwa asilimia 98%,kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
TAMISEMI Bw. Jumanne Sagini.
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Hawa Ghasia
akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini
Dar es salaam uliolenga kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali
yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi wa Serikali uliofanyika jana kote
nchini.
………………………………………………………………………………….
Na: Frank Mvungi- maelezo
Serikali imesema uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika jana
Kote Nchini umefanikiwa kwa Zaidi ya asilimia 98% katika Mikoa yote .
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia wakati wa mkutano na
waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam uliolenga kutoa ufafanuzi
kuhuzi mafanikio ya uchaguzi huo.
Akifafanua Mh. Ghasia amesema kwa kiwango kikubwa wananchi
walijitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi wao katika ngazi ya
Mitaa,Vijiji, na Vitongoji.
Akizungumzia mafanikio ya Uchaguzi huo Mh. Ghasia alitaja Mikoa
ambayo uchaguzi umefanyika katika Halmashauri na Kata zote kuwa ni
Arusha,Mbeya,Kagera,Njombe,Singida,Lindi,Ruvuma,Katavi na Geita.
Mikoa Mingine iliyofanya vizuri katika uchaguzi huo ni
Iringa,Dodoma,Mtawara ambapo Mh. Ghasia aliwapongeza Viongozi na
wataendaji wote wa Mikoa na Halmashauri hizo pamoja na wananchi kwa kazi
kubwa na nzuri waliyofanya hadi kufanikisha uchaguzi huo.
Akitoa ufafanuzi Zaidi kuhusu maboresho yaliyofanywa na
Serikali katika uchaguzi huo Mh. Ghasia amesema kuwa mojawapo ni kuwepo
kwa utaratibu wa kupiga kura kwa kutumia karatasi maalum zilizochapishwa
kitu ambacho katika uchaguzi uliopita hakikuwepo.
Akizungumzia Mikoa ambayo baadhi ya Halmashauri zimeahirisha
uchaguzi ama Halmashauri yote au sehemu ya Kata zake kwa sababu
mbalimbali ikiwemo kuchelewa kufika kwa vifaa vya kupigia kura Mh.Ghasia
aliitaja kuwa ni Kilimanjaro katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo na
Hai,Manyara katika Halmashauri za Hanang na mbulu.
Mikoa Mingine ni Morogoro katika Halmashuri ya Wilaya ya Ulanga
na Mvomero,Mkoa wa Shinyanga Halmashauri ya Wilaya ya Msalala,Mkoa wa
Simiyu Halmashauri ya Wilaya ya Busega na Itilima ambapo Mikoa mingine
ambayo kasoro ndogondogo zilijitokeza na kupelekea uchaguzi kuahirishwa
katika baadhi ya Kata ni Kigoma,Mwanza,Tabora,Tanga,Mara,Rukwa,Pwani na
Dar es salaam.
Akizungumzia Hatua zitakazochukuliwa na Serikali kufuatia
dosari zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo Mh. Ghasia amesema Mikoa
yote imetakiwa awasilishe taarifa rasmi na kamilifu kuhusu
yaliyojitokeza katika Halmashauri zao ambapo Wizara yake itachambua
taarifa hizo ili kubaini chanzo cha kasoro zilizojitokeza ili hatua
stahiki zichukuliwe.
Kuhusu Halmashuri ambazo hazikufanya uchaguzi kutokana na
kasoro mbalimbali Mh. Ghasia amesema kwa mujibu wa Kanuni zinatakiwa
kurudia uchaguzi huo ndani ya siku saba kama kanuni za uchaguzi huo
zinavyoelekeza.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Bw. Jumanne
Sagini alitoa wito kwa vyombo vya habari kuweka uzalendo mbele katika
kuripoti habari za uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kusaidia Taifa
kukamilisha mchakato huo muhimu.
Akifafanua Sagini amesema ni vyema vyombo vya Habari
vikaonyesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika uchaguzi huo pamoja
na kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ngazi ya Mitaa,Vijiji, na
Vitongoji ulifanyika tarehe 14/12/2014 kote nchini ambapo taarifa za
awali zimeonyesha kuwa zoezi la kupiga kura lilienda vizuri katika Mikoa
Mingi.
No comments:
Post a Comment