Na: Anna Nkinda – Maelezo
Watanzania
wengi hawana uelewa wa tatizo la usonji (Autism) kwa watoto hivyo
basi uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa jamii unahitajika ili watu
watambue tatizo hilo na kuweza kuwasaidia watoto hao.
Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais
Mama Salma kikwete wakati akiongea na Prof. Andy Shih ambaye ni Makamu
wa Rais Mwandamizi wa Mambo ya kisayansi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya
Autism Speaks katika ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)
zilizopo jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo alisema jamii ikiwa na uelewa kuhusu watoto
hao kutakuwa na mabadiliko kwa wazazi na walezi hivyo basi ni jukumu la
jamii nzima kuungana na kuweza kuwasaidia watoto hao ili waweze kupata
elimu na mafunzo maalum.
Mwenyekiti huyo wa WAMA
alimpongeza Prof. Shih kwa kazi anayoifanya ya kuwasaidia watoto wenye
usonji Duniani na kwa kitendo chake cha kuamua kuwasaidia watoto wa
Tanzania.
Kwa upande wake Prof. Shih alisema
tatizo la usonji linatibika kama watoto watapewa mafunzo mapema na
jamii ikipata elimu na kulifahamu tatizo hilo itaweza kuwasaidia watu
wenye matatizo hayo kupata huduma.
Alisema alitembelea shule ya
msingi Msimbazi Mseto ambacho ni kitengo mama cha kutoa huduma ya watoto
wenye usonji na kujionea hali halisi na kuahidi kushirikiana na wadau
wengine ili waweze kutatua changamoto zilizopo.
Taasisi ya WAMA kwa kushirikiana
na wadau wa Afya nchini na Taasisi ya kimataifa ya Autism Speaks yenye
makao yake mjini New York Marekani watafanya kazi kwa pamoja ili kutumia
vitendea kazi na utaalam wao ambao wameukusanya kwa miaka mingi
kuwasaidia watoto wenye matatizo ya usonji nchini.
Kazi watakazozifanya ni pamoja na
kuunda timu ndogo ya wataalam wa mitaala na mafunzo ambao watapitisha
miongozo na mitaala iliyopo pamoja na ile ya Autism Speaks na
kupendekeza utaratibu wa mafunzo ya makundi mbalimbali wakiwemo watoa
huduma.
Timu hiyo inaandaa utaratibu wa
mafunzo ya wazazi, walezi na familia ya mtoto mwenye matatizo ya usonji,
kuandaa mwongozo unaokubalika wa kuwapima na kuwatambua watoto wenye
usonji, kuandaa mitaala na miongozo ya ufundishaji wa watoto wenye
usonji na kutumia jukwaa na program za kitaifa kuwalinda watoto.
Wakati wa Mkutano wa 69 wa baraza
kuu la Umoja wa Mataifa (UN) uliofanyika mwishoni mwa mwezi wa tisa
mwaka huu mjini NewYork Marekani Mama Kikwete alikutana na Prof. Shih
ambaye aliahidi kufanya kazi na WAMA ili kuwasaidia watoto wenye tatizo
la usonji ambao wataweza kupata elimu na huduma ya afya kama watoto
wengine.
No comments:
Post a Comment