Mbunge
wa Viti Maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Naomi Kaihula (pichani), amesema tatizo la wakazi wa mabondeni
linatatulika endapo serikali itaweka mikakati mizuri ya miundombinu
katika maeneo hayo.
Kaihula alisema kuwaondoa wakazi hao kwa ajili ya tahadhari
ya mafuriko ni jambo zuri, lakini kwa kuwa wakazi hao wanaishi kihalali
katika maeneo hayo, wanatakiwa kuandaliwa eneo mbadala.
Akizungumza na wakazi wa Jangawani jijini Dar es Salaam juzi,
Kaihula alisema wakati wakazi hao wanajenga nyumba zao katika eneo hilo
serikali ilikuwa inawaangalia, lakini haikuchukua hatua zozote, lakini
sasa ndipo imeona kuwa ni tatizo.
Aliongeza kuwa wapo watu ambao maisha yao yote wamekuwa wakiishi
katika maeneo hayo, hivyo kuanza kuwaondoa bila kuwaandalia maeneo ya
uhakika ni kuwanyanyasa.
Alisema ili kuwasaidia wakazi hao, serikali inapaswa kujenga
nyumba za kisasa na kuweka miundombinu imara katika maeneo hayo
yanayoweza kuhimili mafuriko na kuwapa kipaumbele wakazi hao kuishi
katika nyumba hizo badala ya kuwafukuza kama inavyofanya hivi sasa.
“Suala la serikali kuwaondoa wakazi wa mabondeni kwa ajili ya
tahadhari ya mafuriko ni jema, lakini ni lazima ikumbuke kuwa wakati
wakazi hao wanajenga nyumba zao katika maeneo hayo ilikuwa inawaona na
wapo baadhi ya wakazi ambao wamezaliwa hapo na wamezeekea hapo,
unapowaondoa bila kuwaandalia eneo mbadala ni kuwaonea,” alisema.
No comments:
Post a Comment