Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
akizungumza na Waziri Mkuu wa Qatar , Sheikh Abdullah Nasser Al Thani
kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu huyo iliyopo Doha Desemba 21, 2014. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
Watanzania watanufaika na kipato na maarifa ya teknolojia ya kisasa
kutokana na ajira ambazo watapata katika nchi ya Qatar baada ya mkataba
kusainiwa hivi karibuni.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumapili, Desemba 20, 2014) jijini Doha, Qatar wakati akizumgumza na
waandishi wa habari ili kuwapa taarifa fupi juu ya mambo yaliyojiri
kwenye mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Abdulla Nasser Al
Thani.
Katika mazungumzo hayo ambayo
yalifanyika ofisini kwa Sheikh Abdulla, Waziri Mkuu Pinda amesema
wamekubaliana kutoa ajira kwa Watanzania kwa sababu nchi hii inahitaji
wafanyakazi wengi kwenye sekta mbalimbali na raia wake ni wachache.
“Hivi sasa wapo Watanzania
wanaofanya kazi hapa lakini ni wachache mno. Mazungumzo yalishaanza siku
za nyuma. Tukisaini mkataba katika muda mfupi ujao, tutajua ni idadi
gani wanahitajika na wanaweza kuja kila baada ya muda gani,” alifafanua
Waziri Mkuu.
“Hapa Qatar kuna uwekezaji mkubwa
umefanyika, kwa hiyo wanahitaji watu wa kufanya kazi… kwenye mahoteli,
viwandani, na kikubwa hapa ninachokiona watu wetu watapata kipato lakini
pia watapata ujuzi kwa maana ya maarifa yanayoendana teknolojia ya
kisasa,” aliongeza.
Akeleza mambo mengine ambayo
wamekubalina kushirkiana kama nchi rafiki, Waziri Mkuu alisema kuna
mambo makuu manne likiwemo hilo la ajira. “La kwanza ni Kilimo. Hapa
Qatar ni jangwa kila mahali. Wamekubali kuja kuwekeza kwenye kilimo,
ufugaji na uvuvi kwa sababu sisi tuko karibu nao zaidi kuliko Marekani
au Brazil.”
“Wanaweza kupata mchele, matunda,
nyama kwa maana ya machinjio na viwanda vya kusindika nyama lakini pia
katika uvuvi wa samaki. Tunayo bahari ila mitaji yetu ni midogo. Kwa
hiyo wamekubali kuangalia eneo hilo pia,” alisema.
Alisema eneo la pili ni la gesi na
mafuta. “Wamekubali kutusaidia utaalmu ili tushirikiane nao katika
namna kutumia gesi kwenye ngazi ya chini hasa viwanda kwa sababu wenzetu
wana uzoefu wa muda mrefu. Hata kwenye mafuta wameonyesha kuwa wako
tayari,” alisema.
Eneoa la tatu alilitaja kuwa ni
kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania na la nne ni TEHAMA. “Hawa wenzetu
wamechanganya TEHAMA na sayansi na sasa wana Jiji la Sayansi na
Teknolojia. Chini ya makubaliano tutakayofikia, watu wetu watakuja
kujifunza masuala ya gesi na mafuta.”
Alisema wamekubaliana na Sheikh
Abdulla al Thani kuunda timu ya pamoja baina ya nchi zao ili ifanye kazi
ya kuainisha ni maeneo gani wanataka waanze nayo kwanza kulingana na
mahitaji. “Nimemuahidi nikifika nyumbani nitaandika barua ili mchakato
wa kuunda timu uanze rasmi,” alisema.
Mchana huu, Waziri Mkuu Pinda
atakuwa na mazungumzo ya Kiserikali na Mawaziri wa Kazi na Ustawi wa
Jamii; Uchukuzi; Miundombinu na Uwekezaji wa Qatar. Naibu Mawaziri
atakaokutana nao ni wa Uchumi na wa Nishati.
Jioni Waziri Mkuu amepangiwa
kukutana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Qatar (Qatar
Business Community), wajumbe wa Chama cha Wafanyabiashara cha Qatar
(Chamber of Commerce of the State of Qatar) na pia atakutana na
Watanzania waishio Qatar. Kesho (jumatatu, Desemba 22, 2014) atatembelea
Mamlaka ya Bandari ya Qatar na makao makuu ya kampuni ya uchimbaji gesi
ya Qatar.
Waziri Mkuu amefuatana na Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kimani; Waziri wa Kilimo na
Maliasili wa Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim; Naibu Waziri wa
Nishati, Bw. Charles Kitwanga; Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Bw. Godfrey Zambi.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Bw. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Halima Dendego, wabunge
wawili Bi. Amina Makilagi na Bw. Aeshy Hilali, Dk. Gideon Kaunda wa TPSF
na Bw. Shigela Malocha kutoka TPDC.
No comments:
Post a Comment