Na Anna Nkinda –
Maelezo, Lindi
14/12/2014 Vijana wa wilaya ya Lindi mjini wametahadharishwa kutokubali kudanganywa na kutumiwa kufanya vurugu ambazo zinaharibu vitu vichache walivyonavyo na kwa kufanya hivyo wanarudisha nyuma maendeleo yao.
14/12/2014 Vijana wa wilaya ya Lindi mjini wametahadharishwa kutokubali kudanganywa na kutumiwa kufanya vurugu ambazo zinaharibu vitu vichache walivyonavyo na kwa kufanya hivyo wanarudisha nyuma maendeleo yao.
Tahadhari hiyo imetolewa jana na
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kupitia wilaya hiyo Mama Salma Kikwete wakati akiwanadi wagombea wa
chama hicho kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa Wenyeviti
na Wajumbe wa Serikali za mitaa uliofanyika katika Kata ya Makonde.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema ni vyema vijana wakaelewa
historia ya nchi yao na kujua lipi jema na baya kwani kuna baadhi ya
wanasiasa wanawashawishi ili wafanye vurugu kwa madai kuwa hakuna
maendeleo yoyote yaliyopatikana jambo ambalo siyo kweli.
“Hao wanaowadanganya nyinyi
mfanye vurugu na kuharibu vile vichache mlivyonavyo eti kwa kuwa maisha
yenu hayajaimarika kwao hawafanyi hivyo, kwao kuna maendeleo na ninyi
mnazidi kujirudisha nyuma kimaendeleo. Msikubali mkoa wetu uwe sehemu
ya majaribio na kutumika kwa manufaa yao”.
Kama wangekuwa wanawapenda na
kutaka kuwasaidia ili muendelee wangewajengea hata shule ambazo
zingewafanya vijana na watoto wetu wasome, hapo hakuna kipingamizi kwani
Elimu ni mkombozi wa maisha na elimu inaleta maendeleo”, alisema Mama
Kikwete.
MNEC huyo alisema Serikali makini
ni lazima ijali maisha ya watu wake, kwa kutambua hilo Serikali ya CCM
imeimarisha miundo mbinu kwa kujenga barabara za lami, shule ili watoto
wasome na kuimarisha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kujenga
Hospitali na vituo vya afya na kuhakikisha wahudumu wa afya
wanaongezeka.
Alisema, “Maisha bora kwa kila
mtanzania siyo Chama kinapita nyumba kwa nyumba kugawa pesa bali ni kwa
kuboresha miundombinu, kukiwa na shule watoto watasoma, kukiwa na
barabara nzuri wananchi wasafirisha mazao yao, kukiwa na huduma bora za
afya wananchi watatibiwa haya yakifanikiwa maisha ya mtu mmoja mmoja
yataimarika”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM
wilaya ya Lindi Mjini Muksini Rafii alisema katika uchaguzi huo ndani
ya wilaya hiyo wagombea za nafasi za wajumbe 147 na wenyeviti saba
wamepita bila kupingwa.
Kwenye mkutano huo mwanachama
mmoja aliyejulikana kwa jina la Raphael Mahuna kutoka Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye alikuwa ni mgombea wa nafasi
ya Mwenyekiti wa mtaa wa National Housing kwa tiketi ya chama hicho na
mwanachama mmoja kutoka Chama cha Wananchi (CUF) walijiunga na Chama
Cha Mapinduzi.
Mahuna alisema ameamua kwa hiari
yake mwenyewe bila ya kulazimishwa kujiunga na CCM kwani alipokuwa
anagombea nafasi ya Mwenyekiti wa mtaa wa National Housing alishindwa
kufanya kampeni kwa kuwa alikosa wajumbe wa kumuunga mkono.
Katika uchaguzi wa Serikali za
mitaa, vijiji na vitongoji mkoani Lindi wagombea wa Chama Cha Mapinduzi
katika vitongoji 600, vijiji 87 na mitaa nane wamepita bila kupingwa.
No comments:
Post a Comment