Dar es salaam.
Jamii imetakiwa kuendelea
kuunga mkono juhudi za Serikali za ujenzi wa mabweni katika shule za
Sekondari zilizoko pembezoni mwa miji hasa maeneo ya vijijini ili
kukabiliana na tatizo la msongamano wa wanafunzi mijini linalosababishwa
na baadhi ya wanafunzi kushindwa kujaza nafasi wanazopangiwa maeneo
ya pembezoni mwa miji kutokana na umbali.
Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini
Dar es salaam na Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es salaam Bi. Theresia
Mmbando wakati akizungumza na viongozi wa Elimu wa mkoa na walimu wakuu
wa Shule za Sekondari za mkoa wa Dar es salaam wakati wa kikao cha
Kamati ya Uchaguzi wa wanafunzi wa watakaojiunga na kidato cha kwanza
mwaka 2015.
Alisema mwaka huu mkoa wa Dar
es salaam umekuwa na kiwango cha juu cha ufaulu kitaifa kwa kuwa na
wanafunzi wanaokidhi vigezo vya kuendelea na masomo ya sekondari kwa
kiwango cha asilimia 78 ukifuatiwa na mkoa wa Kilimanjaro ambao umepata
asilimia 69.
Alifafanua kuwa kati ya
wanafunzi 60,709 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kumaliza Elimu ya
Msingi mwaka huu , wanafunzi 59,577 ambao ni sawa na asilimia 98.14
waliofanya mtihani huo, wavulana wakiwa 28,419 na wasichana 31,158.
Bi. Mmbando alibainisha kuwa
kati ya hao watahiniwa 1,132 sawa na asilimia 1.86 katika mkoa wa Dar
es salaam hawawakuweza kufanya mtihani huo kutokana sababu mbalimbali
zikiwemo utoro, vifo, ugonjwa na sababu nyinginezo.
Akizungumzia kuhusu ufaulu wa
wanafunzi hao kimkoa alisema wanafunzi 46,434 sawa na asilimia 78
walifaulu mtihani huo na kuufanya mkoa wa Dar es salaam kuongoza kwa
kuwa na ufaulu wa juu kitaifa wavulana 22,389 na wasichana 24,086.
Alibainisha kuwa wanafunzi
36,610 walichaguliwa katika chaguo la kwanza kujiunga na shule
mbalimbali za Sekondari za ndani na nje ya mkoa wa Dar es salaam na
kufafanua kuwa wanafunzi 9824 waliobaki sawa na asilimia 21 ambao nao
wamefaulu watachaguliwa katika chaguo la pili kufuatia baadhi ya
wanafunzi waliochaguliwa katika chaguo la kwanza kujiunga na shule
zisizokuwa za serikali na nafasi zao kubaki wazi.
Katika kufanikisha zoezi hilo
Bi. Mmbando alieleza kuwa mkoa tayari umeunda timu tatu zitakazofuatilia
idadi ya wanafunzi watakaoshindwa kufika katika shule walizopangiwa
kuanzia Januari 14, 2015 katika halimashauri za Temeke, Ilala na
Kinondoni ili nafasi zao zijazwe na wanafunzi wengine.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa
Mkoa wa Dar es salaam Bw. Raymond Mapunda akitoa tathmini ya mtihani wa
kumaliza Elimu ya Msingi uliofanyika nchi nzima mwezi Septemba mwaka huu
alisema mkoa wake ulifanya vizuri kutokana na juhudi za walimu pamoja
na wanafunzi kuuelewa vizuri mfumo wa ufanyaji mitihani uliotumika wa
Optical Mark Reader (OMR).
Alisema kuwa wanafunzi wa shule
506 za jiji la Dar es salaam walifanya mtihani walitumia mfumo huo kwa
ufanisi mwanafunzi 1 alifutiwa matokeo yake kwa sababu za udanganyifu, 2
walipata alama 0 huku wavulana 10 na wasichana 10 kutoka wilaya ya
Ilala na Kinondoni waliibuka washindi wa nafasi 10 bora kitaifa.
No comments:
Post a Comment