Katibu
 wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Ndugu Nape Nnauye akizungumza na waandishi
 wa habari leo asubuhi katika ofisi kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar juu 
ya ratiba ya mchakato wa kupata wagombea  ndani ya chama katika uchaguzi
 ujao na kikao cha kamati ndogo ya maadili ya CCM iliyofanya kikao chake
 jana na kujadili suala la wanaotuhumiwa kuhusika katika sakata la 
akaunti ya Tegeta Esrow ambapo amesema taarifa ya kikao hicho itapelekwa
 kwenye kamati kuu kamataratibu za chama zinavyosema na kamati kuu 
itatoa taarifa kwa wananchi.   
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
……………………………………………………………………
Mwaka huu 2015 ni mwaka wa 
uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge, Rais wa Serikali ya Mapinduzi 
Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Hii ni kwa mujibu wa katiba ya 
nchi. Ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM kwa nafasi hizo 
haijatolewa bado.
Itakumbukwa Kamati Kuu iliyopita 
ya tarehe 13/01/2015, iliyoketi Kisiwandui Zanzibar ilipitisha ratiba ya
 shughuli za kawaida za Chama kwa mwaka 2015 na kupanga kushughulikia 
ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM vikao vijavyo.
Pamoja na kutotolewa kwa ratiba 
hiyo, bado zimekuwepo harakati nyingi za wanaotaka kuteuliwa na CCM 
kugombea nafasi mbalimbali hasa ya urais wa Jamhuri ya Muungano. 
Harakati hizo baadhi halali, nyingi haramu.
Pamoja na kutaadharishwa mara 
nyingi juu ya madhara ya harakati hizo kwa umoja na mshikamano wa Chama 
bado baadhi yao wamekuwa wakiendelea na harakati hizo.
Kwa muda sasa kumekuwepo na uzushi
 mwingi juu ya baadhi ya wanaotaka kuwania nafasi hizo kujadiliwa na 
hata kuchukuliwa hatua na vikao vya chama. Maneno haya kwa sehemu kubwa 
yamekuwa yakisambazwa na wagombea wenyewe au wapambe wao.
Uzushi huu, hauna nia njema kwa 
CCM, unalengo la kukigawa Chama na kuonyesha kama vile Chama hakina kazi
 nyingine ila kujadili na kushughulika na watu hao. Kwa mara nyingine 
CCM inapenda kuwataadharisha wagombea hao na wapambe wao kujiepusha na 
kusambaza taarifa zisizokuwa za kweli. Kwa kuwa vitendo hivi vinakigawa 
Chama chetu.
CCM haitasita kuchukua hatua kali 
dhidi ya wote wanaosambaza taarifa hizi. Ni vyema wagombea wakawadhibiti
 wapambe wao na wakajichunga wenyewe dhidi ya hujuma hizi kwa Chama 
kwani zitawapotezea sifa ya kugombea.
Wengi wa wanaosambaza taarifa hizi
 ni wagombea au wapambe wasiojiamini kutokana na matendo yao, ambayo 
hata wao wana mashaka na uadilifu wao. Hatuoni sababu ya mgombea 
anayefuata sheria, kanuni na taratibu za Chama kuhofia kuchukuliwa hatua
 kila vikao vya Chama vinapofanyika.
Ukitenda kwa haki huna haja ya kuogopa vikao na kuzusha uongo na uzushi usio na ukweli. CCM inaamini matendo haya hayatajirudia.
Aidha Chama Cha Mapinduzi 
kinawaomba wanachama na wananchi kuzipuuza taarifa zinazosambazwa kwa 
kuvinukuu vyanzo visivyo rasmi, kama kuna hatua au taarifa kwa umma juu 
ya hatua yoyote katika mchakato huu basi itatolewa na wasemaji halali wa
 Chama na si kutoka vyanzo vya barabarani.
Itakumbukwa pia baada ya Kamati 
Kuu iliyopita kukutana tulitangaza kufanyika kwa kikao cha Kamati Ndogo 
ya Maadili kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kimaadili kwenye sakata
 la Escrow kwa viongozi wa Chama walioko kwenye vikao vya Chama vya 
maamuzi.
Jana kumekuwepo na harakati nyingi
 za vyombo vya habari na watu binafsi kujaribu kupata taarifa ya nini 
kimetokea kwenye kikao hicho cha Maadili.
Tunapenda kuwakumbusha kuwa kwa 
mujibu wa taratibu taarifa za kilichotokea kwenye kikao cha Kamati Ndogo
 ya Maadili huwa hazitolewi kwa umma mpaka baada ya kufikishwa kwenye 
Kamati Kuu. Hivyo basi tunawaomba kutulia na kusubiri taarifa rasmi 
baada ya kufikishwa kwenye Kamati Kuu kuliko kuhangaika sasa hivi, jambo
 linaloweza kusababisha kuokotwa kwa habari za barabarani ambazo nyingi 
si za kweli. Tulieni subirini taarifa rasmi.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi.
20/01/2015
No comments:
Post a Comment