Mkuu
 wa Mkoa wa Lindi Mwantumu Mahiza akiwakaribisha wajumbe wa kamati ya 
Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji waliotembelea mkoa huo kukagua baadhi ya
 miradi ya Maji iliyopo mkoani humo.
Kiongozi
 wa ziara ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Amina
 Makilagi akieleza lengo la ziara ya kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo 
na Maji mkoani Mtwara kwa Mkuu wa mkoa huo Mwantumu Mahiza 
(kushoto).Kulia ni mjumbe wa kamati hiyo Asaa Hamadi.
Mwenyekiti
 wa Halmashauri ya Lindi Mathei Makwinya, akieleza jambo wakati ziara 
ilipowasili kwenye kijiji cha Mnara kukagua mradi wa Rondo-Mnara.Kulia 
kwake ni Kiongozi wa wajumbe wa kamati ya Bunge, Amina Makilagi, Mkuu wa
 wilaya ya Lindi Nassor Himid na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya 
Lindi Olliver Vavunge.
Baadi
 ya viongozi wa kijiji na kamati ya maji ya kijiji cha Mnara na Chiponda
 wakimsikiliza Kiongozi wa ziara ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya 
Kilimo, Mifugo na Maji, Amina Makilagi (hayupo pichani).
 Kiongozi wa ziara ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na 
Maji, Amina Makilagi, akizungumza na viongozi wa mradi wa maji wa 
Rondo-Mnara na kata ya Mnara.
Mhandisi
 wa Maji mkoa wa Lindi Valentine Ndyano (aliyevaa shati la kitenge) 
akifafanua jambo kwa wajumbe wa kamati ya Bunge kuhusu mtambo wa 
kusukuma maji.
Mhandisi
 wa Maji mkoa wa Lindi Valentine Ndyano akifafanua jambo kwa wajumbe wa 
kamati ya Bunge kuhusu mtambo wa kusambaza maji kwenye vituo vya maji.
Kiongozi wa wajube wa kamati akizingumza na wananchi wa kijiji cha Mnara baada ya kukagua mradi wa maji wa Rondo-Mnara. 
Wajumbe wakikagua maendeleo ya mradi huo unaotarajiwa kukamilika Machi mwaka huu.
…………………………………………………………………….
Hussein Makame, MAELEZO, Lindi
WANANCHI waliopo kwenye maeneo ya 
miradi ya maji mkoani Lindi na nchini kwa ujumla wametakiwa kuacha 
kuzembea kwenye vikao vya kujadili maendeleo ya miradi hiyo kwani 
kufanya hivyo kutachangia kufa kwa miradi hiyo.
Hayo yamesemwa na Kiongozi wa ziara
 ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji mkoani Pwani, 
Lindi na Mtwara Amina Makilagi (Mb) wakati alipotembelea mradi wa maji 
wa Rondo-Mnara uliopo katika kijiji cha Mnara Kata za Mnara na Chiponda 
wilaya ya Lindi mkoani Lindi.
Alisema miradi mingi ya maendeleo 
imekufa kutokana na wananchi kuzembea kwenye vikao vya kujadili 
uendeshaji wa miradi ya maji, hivyo kuwafanya viongozi wasio waaminifu 
kutumia vibaya fedha za miradi hiyo.
“Mnachotakiwa msizembee kwenye 
vikao vya kujadili miradi ya maji kwani mkifanya hivyo miradi itakufa 
kutokana na viongozi kutumia vibaya fedha za miradi hiyo kujinufaisha 
wenyewe” alisema Makilagi.
Alisema wanatakiwa kuhakikisha kuwa
 wanasimamia utaratibu wa kuingiza fedha za miradi ya maendeleo ya maji 
kwenye akaunti kwani kufanya hivyo kutaepusha viongozi wabadhirifu 
kuihujumu miradi hiyo.
Akisoma taarifa ya mradi huo mbele 
ya wajumbe wa kamati hiyo ya bunge, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya 
Lindi Olliver Vavunge alisema mradi wa Rondo-Mnara ulisanifiwa kuhudumia
 wakazi 18,000 kwenye vijiji sita.
Alisema mradi huo uliojengwa na 
serikali mwaka 1973 una uwezo wa kuzalisha mita za maji zenye ujazo wa 
450 kwa siku lakini kutokana na changamoto ya uchakavu wa mitambo na 
gharama kubwa za uendheshaji, uzalishaji umepungua hadi mita za ujazo 
328 kwa siku.
 “Vituo vitatu vya kusukua maji 
vilijengwa kutoka kwenye chanzo cha maji kilichopo katika kijiji cha 
Chikote.Ambapo kwenye kila kituo ilifungwa mitambo miwili ya kusukuma 
maji iliyotumia injini ya diseli.” Alisema Vavunge.
Alisema mradi wa Rondo-Mnara ni 
miongoni mwa miradi minne ya maji safi na salama ambayo hadi sasa 
imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi ikiwemo miradi ya Kiwawa, 
Likwaya na Namkongo.
“Miradi hiyo inatoa huduma ya maji 
kwa wakazi 5,000 huku halmashauri ikiendelea kutekeleza miradi ya Maji 
ya Namangale, Hingawali, Littipu, Nyangamara na Nahukahuka” alisema.
Kwa upande wa mradi wa Ng’apa 
unaojulikana kwa jina la 7 Towns Upgrading Program, unaofadhiliwa na 
serikali ya Ujerumani na Jumuiya ya Ulaya, una lengo la kuboresha huduma
 ya maji katika mji wa Lindi.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika 
mwezi Machi mwaka huu na kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa 
wakazi 194,143 wa manispaa ya Lindi na unajenga mtambo wa kusafisha 
majitaka yanayozalishwa katika mji wa Lindi.
Awali akiwasilisha taarifa ya 
huduma ya maji mkoa wa Lindi kwa wajumbe wa kamati hiyo ya Bunge mkoani 
Lindi, Afisa Tawala wa Mkoa wa Lindi Abdallah Chikota alisema hadi 
Novemba mwaka 2014 wakazi wa mijini wanaopata maji safi ni asilimia 55.4
 ya wakazi wote 162, 049.
Alisema kwa upande wa wakazi wa 
vijijini wanaopata huduma ya maji safi na salama wanakadiiriwa kufikia 
297,796 kati ya wakazi 702, 603 wa vijijini.
Naye Mkuu wa mkoa wa Lindi Mwantumu
 Mahiza alisema pamoja na Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kutoa huduma
 ya maji safi na salama kwa wakazi wa mkoa huo, lakini huduma hiyo 
haipatikani kama inavyotakiwa kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme 
ambao kwa siku unaweza kukatika kati ya mara 22 hadi 25.
Hata hivyo, alisema amewasilisha 
taarifa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na wanatarajia kukutana 
na uongozi wa juu wa shirika hilo hivi karibuni ili kujadili changamoto 
hiyo ambayo inategemewa kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa maji 
mkoani humo.
Ziara ya wajumbe wa kamati ya Bunge
 ya Kilimo, Mifugo na Maji inaendelea kukagua miradi ya maji katika mkoa
 wa Mtwara ambapo inatarajia kukagua miradi ya Nanyamba-Namkuku na 
Tandahimba-Matogolo.
No comments:
Post a Comment