Katibu
 Msaidizi Idara ya Ajira kutoka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira 
katika Utumishi wa Umma Bw. Malimi Muya akiwaeleza waandishi wa Habari 
leo jijini Dar es salaam (hawapo pichani) sababu zinazopelekea Vijana 
wengi kupenda kufanya kazi katika Utumishi wa Umma ikiwemo uboreshaji wa
 mishahara,kuboreshwa kwa mazingira ya kazi,usalama wa kazi unaotokana 
na kuwepo kwa taratibu za kazi zinazotabirika ,kuwepo kwa taratibu 
maalum zinazomhakikishia mwajiriwa maslahi au malipo bora baada ya 
kuhitimisha ajira yake.kushoto ni Afisa Habari wa Sektetarieti hiyo Bw. 
Kassim Nyaki na kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bw. 
Frank Mvungi. 
Afisa
 Habari toka Ofisi ya Rais Sektetarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
 Bw. Kassim Nyaki akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo 
pichani) wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es 
salaam,Katikati ni Katibu Msaidizi Idara ya Ajira kutoka Ofisi ya Rais 
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Malimi Muya na kulia 
ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Frank Mvungi.           
Baadhi
 ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Katibu Msaidizi Idara ya Ajira 
kutoka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. 
Malimi Muya leo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano uliolenga kutoa 
taarifa ya mafanikio ya Sekretarieti hiyo ikiwemo kuwapangia vituo vya 
kazi jumla ya waombaji kazi 12,858 walioshinda usaili kufikia Novemba 
2014.
(Picha zote na Idara ya Habari Maelezo )
……………………………………………………………………………………
Frank Mvungi- Maelezo
Serikali imewapangia vituo vya kazi waajiriwa 12,858 katika 
Utumishi wa Umma kufikia Novemba mwaka 2014 ambao walifuzu usaili 
kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya ajira katika Utumishi wa Umma.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Katibu Msaidizi Idara
 ya Ajira kutoka Sekretarieti hiyo Bw. Malimi Muya wakati wa mkutano na 
Waandishi wa habari uliolenga kueleza mafanikio ya Sekretarieti hiyo 
hadi mwishoni mwa mwaka jana.
Akizungumzia suala la maombi ya ajira yaliyowasilishwa katika 
Sekretarieti hiyo, Muya alibainisha kuwa jumla ya barua za maombi 
191,844 zilifikishwa na kupokelewa na Sekretarieti hadi Septemba 2014 
ambapo jumla ya waombaji 71,124 walikidhi vigezo na waliitwa kwenye 
usaili baada ya uchambuzi kufanyika.
“Kati ya waombaji 71,124 waliotwa kwenye usaili huo, ni waombaji
 12,858 ndio waliofuzu na waliopangiwa vituo vya kazi ambapo wanaume 
walikuwa 7,598 sawa na asilimia 59.1 na wanawake walikuwa 5,260 sawa na 
asilimia 40.9.” alisisitiza Muya.
Aidha kati ya waajiriwa 12,858 waliopangiwa vituo vya kazi Muya 
alibainisha kuwa Vijana wenye umri kati ya miaka 21-25 ni 1045 sawa na 
asilimia 8.1 wenye umri kati ya miaka 26-30 ni 6,346 sawa na asilimia 
49.4 ambapo kati ya mwaka 2010 hadi 2014 utumishi wa umma umeajiri 57.5 
ya vijana wenye umri wa miaka 21-30.
Akizungumzia sababu zinazowavutia na kuwasukuma vijana kuingia 
katika Utumishi wa Umma, Muya alisema kuwa uboreshaji wa mishahara, 
kuboreshwa kwa mazingira ya kazi, usalama wa kazi unaotokana na kuwepo 
kwa taratibu za kazi zinazotabirika ndizo mojawapo ya sababu 
zinazowavutia vijana wengi kuomba kazi katika utumishi wa umma..
Sababu nyingine zinazowavutia vijana kupenda kuajiriwa katika 
utumishi wa umma ni kuwepo kwa mabadiliko ya mara kwa mara ya kanuni na 
taratibu za kazi zinayofanywa kukidhi mahitaji ya watumishi kwa wakati 
unaohusika, kuwepo kwa taratibu maalum zinazomhakikishia mwajiriwa 
maslahi bora baada ya kuhitimisha ajira yake.
Akizungumzia kada zenye fursa pana ya ajira, Muya alisema kuwa 
kada ya gesi, petrol, Madaktari wa mifugo, wahandisi, na mafundi mchundo
 katika sekta za maji,umeme na afya,hivyo kuwataka vijana kusoma masomo 
ya Sayansi.
Aidha Muya alitoa wito kwa wale wote ambao wameshapangiwa vituo 
vya kazi katika Utumishi wa Umma kujituma, kuwa wabunifu katika sehemu 
zao za kazi kwani Taifa linawategemea vijana katika kufikia maendeleo 
endelevu kwa manufaa ya sasa na ya baadae.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Sekretarieti hiyo Bw. Kassim 
Nyaki alibainisha kuwa waombaji kazi waliofanya usaili mwezi Desemba, 
2014 kuwa waliofaulu na kupangiwa vituo vya kazi jumla yao ni 572 ambapo
 watapangiwa vituo hivyo kabla ya mwisho wa mwezi Januari 2015.
No comments:
Post a Comment