Na Anna Nkinda – Lindi
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete 
amewataka wakazi wa Kata ya Ng’apa wilaya ya Lindi mjini kuchagua 
viongozi waadilifu na wenye sifa ambao watawaongoza wananchi kusimamia 
shughuli za maendeleo yao.
Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa 
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia 
wilaya ya Lindi mjini alitoa rai hiyo jana wakati akiongea na wananchi 
waliohudhuria mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa 
Serikali za mitaa uliofanyika katika Kata hiyo.
Mama Kikwete alisema kuna baadhi 
ya watu wanachagua viongozi kwa ushabiki pasipo kuangalia kiongozi huyo 
kama ana sifa au la, na kuwasisitiza wananchi hao  siku ya uchaguzi 
ikifika wasifuate mambo ya ushabiki na kuchagua kiongozi kwani ushabiki 
hauna manufaa yoyote.
“Nawaombeni muwapigie kura za 
ndiyo viongozi wote wa  CCM wanaogombea nafasi za Wenyeviti na Wajumbe 
wa Serikali za Mitaa,  kwani hawa wanasifa na mkiwachagua kutakuwa  na 
manufaa kwenu na vizazi vyenu hivyo basi wote mliojiandikisha  siku ya 
uchaguzi ikifika mjitokeze  kupiga kura na kukichagua  Chama chetu”, 
alisema .
Aidha MNEC huyo aliwakumbusha 
wanachama wa CCM siku ya uchaguzi kutokwenda kupiga kura wakiwa wamevaa 
sare za Chama au mavazi yoyote yenye kuonyesha ushabiki wa Chama cha 
siasa hiyo hairuhusiwi na kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Maadili
 ya vyama vya Siasa na Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi .
Kuhusu elimu Mama Kikwete alisema 
Serikali ya CCM kwa kushirikiana na wananchi imefanikiwa kujenga shule 
za Sekondari nchi  nzima na ifikapo mwakani maabara kwa ajili ya masomo 
ya sayansi katika shule hizo zitakuwa zimekamilika na kuanza kutumika.
Alisema, “Ninawaomba wazazi na 
walezi msimamie watoto waende shule ili wawe na maisha bora hapo baadaye
 kwani tatizo  kubwa lililoko hapa ni watoto kutokwenda shule. Serikali 
imewajengea shule na maabara lakini kama watoto wenu  hawataenda shule 
ni kazi bure, ili shule hizi ziwe na faida kwenu ni lazima watoto wenu 
wasome”.
Mama Kikwete pia alitembelea Kata 
ya Makonde na kuongea na wanachama pamoja na wagombea wa nafasi za 
Uenyeviti na Wajumbe na  kuwapongeza viongozi wa zamani ambao wanamaliza
 kipindi chao cha uongozi kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutekeleza na 
kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi. 
Aliwapongeza wanawake 
waliojitokeza na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi jambo ambalo 
litawawezesha  kuingia katika ngazi ya maamuzi.
Mama Kikwete yupo wilayani humo 
kwa ajili ya shughuli za kichama ikiwa ni pamoja na kushiriki  kwenye 
kampeni na kuwanadi wagombea wa chama hicho wanaowania nafasi mbalimbali
 za uongozi katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na 
Vitongoji  utakaofanyika tarehe 14 mwezi huu.

No comments:
Post a Comment