Waandishi Wetu MCHUNGAJI
 Kiongozi wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God jijini Dar, Dk. 
Getrude Rwakatare (pichani) amefunguliwa mashitaka katika Kituo cha 
Polisi Wazo Hill kwa uharibifu wa mali inayodaiwa ina thamani ya 
shilingi milioni 20.
Taarifa zilizopatikana katika kituo hicho zenye Jalada la Kumbukumbu 
WH/RB/9029/2014 UHARIBIFU WA MALI na kuthibitishwa na mlalamikaji 
aliyejitambulisha kwa jina la Grayson Justine, zinaeleza mchungaji huyo 
alivunja nyumba ya Grayson kwa greda hali iliyomfanya mmiliki huyo 
kuzimia na kulazwa Zahanati ya Mico iliyopo Wazo Hill baada ya presha 
kupanda.
Katika mahojiano na waandishi wetu katika Ofisi za Global Publishers,
 Bamaga- Mwenge, Dar wiki iliyopita, Grayson alikuwa na haya ya kusema:
“Kiwanja nilichojengea nyumba nilikinunua kwa Jumanne Rajab, Agosti 
24, 2011 na makubaliano yalifanyika kwa kuandikishiana Ofisi za Serikali
 ya Mtaa wa Bunju ‘B’ na kila mmoja alikuwa na mashahidi wake.
“Kutokana na kuchoka katika kupangisha, niliamua kuchukua mkopo wa 
shilingi milioni 20 kazini ili nijenge haraka na kuhamia, ujenzi ulianza
 Septemba 21,  mwaka 2013 mpaka kufikia mwezi huu (Novemba) nilibakiza 
kupaua na nilitarajia kuhamia mwanzoni mwa mwaka kesho.
“Baadaye nilikwenda Moshi kwenye msiba wa baba, niliporudi Dar 
nilimaliza siku moja tu, nikaripoti kazini. Nikiwa kazini Novemba 11, 
mwaka huu nikapigiwa simu na jirani kwamba nyumba yangu inabomolewa na 
greda, alifikiri kwamba nimeshaonana na Mchungaji Rwakatare na 
kukubaliana naye.
“Nilikwenda kule, kufika nikakuta hakuna jengo! Nilidondoka chini, 
sikujua kilichoendelea, nilipoteza fahamu, nilijitambua nikiwa Zahanati 
ya Mico.
“Kinachoniumiza sana ni kitendo cha 
kuvunjiwa nyumba yangu bila kushirikishwa, bora hata angenifungulia 
mashitaka kama anaona nilivamia kikwanja chake.”
“Yeye ana uwezo, ana ghorofa ya zaidi ya shilingi bilioni moja iweje anionee na kunivunjia mimi maskini niliyejenga kwa fedha za mkopo?
“Yeye ana uwezo, ana ghorofa ya zaidi ya shilingi bilioni moja iweje anionee na kunivunjia mimi maskini niliyejenga kwa fedha za mkopo?
“Kituo cha polisi nilifika karibu mara nne lakini mpaka leo hii 
sijapewa mpelelezi wala hawajafika eneo la tukio, nataka sheria ichukue 
mkondo wake.”
Mwandishi alifika katika eneo la tukio na kushuhudia kifusi 
kinachodaiwa kuwa ni iliyokuwa nyumba ya Grayson iliyovunjwa na 
imezungushiwa ukuta na geti kupigwa kufuli.
Hata hivyo, Uwazi lilifika katika Ofisi za 
Serikali ya Mtaa wa Bunju ‘B’ na kuonana na mtendaji Abdallah Mkeyenge 
ambaye alikiri kuwepo kwa mvutano baina ya watu hao.“Hii barua ya 
makubaliano ya kuuziwa Grayson kiwanja inaonekana imetoka ofisini hapa 
lakini mimi kipindi hicho nilikuwa sijahamia ofisi hii.
“Ninachokumbuka kuna kipindi Mchungaji Rwakatare alikuja na milioni 
tano kuwapa Grayson na mtu mwingine yaani kuwapoza lakini walikataa 
kuzichukua,” alisema mtendaji huyo.
Mchungaji Rwakatare alipopigiwa simu kuhusiana na madai hayo alisema 
yupo bungeni hivyo alimwagiza msaidizi wake, Jerad Abeid kuzungumzia 
sakata hilo ambapo alisema eneo hilo mchungaji analimiliki  tangu mwaka 
2005 na hati ziko ardhi Wilaya ya Kinondoni. Alibomoa nyumba ya Grayson 
akijua ni eneo lake la siku nyingi.
“Unajua katika maeneo hayo kuna watu walikuwa wakishirikiana na ofisi
 za mtaa kuuza kiwanja cha mchungaji kwa siri na tayari watu wanne 
walishauziwa lakini walikuwa hawajajenga,  mchungaji aliamua kuwapoza 
kiubinadamu na wameshaondoka bado watu wawili akiwemo huyo Grayson,” 
alisema Jerad.






No comments:
Post a Comment