Shirikisho la Mpira wMiguu 
Tanzania (TFF) limeitaka mikoa mitano kuwasilisha usajili wa wachezaji 
wake kwa ajili ya mashindano ya Taifa ya Copa Coca-Cola 2014 kabla ya 
Desemba 5 mwaka huu.
Mikoa hiyo ambayo haijawasilisha 
usajili wake hadi sasa kwa ajili ya michuano hiyo inayoanza Desemba 13 
mwaka huu jijini Dar es Salaam ni Arusha, Dodoma, Katavi, Kusini Pemba, 
Kusini Unguja, Mjini Magharibi na Simiyu.
Kwa mujibu wa Kamati ya Mashindano
 ya michuano hiyo, mkoa ambao hautawasilisha usajili wake kwa ajili ya 
uhakiki wa umri wa wachezaji utakaonza Desemba 10 mwaka huu utaondolewa 
katika fainali hizo zitakazomalizika Desemba 20 mwaka huu.
Wachezaji watakaobainika kuzidi 
umri hawataruhusiwa kushiriki katika michuano hiyo inayoshirikisha 
wachezaji wenye umri chini ya miaka 15. Kwa mujibu wa Kanuni ya 29 ya 
michuano kuhusu idadi ya wachezaji, kila timu inatakiwa kuwa na 
wachezaji wasiozidi 20 na wasiopungua 16.
Hivyo, kila timu inatakiwa 
kuhakikisha inakuwa na idadi hiyo ya wachezaji, kwani kikanuni 
wakipungua 16 itaondolewa kwenye mashindano.
Timu 16 kwa upande wa wavulana 
zitashiriki katika fainali hizo wakati kwa upande wa wasichana ni timu 
nane. Mikoa iliyoingiza timu za wasichana kwenye fainali hizo ni Arusha,
 Dodoma, Ilala, Kinondoni, Mbeya, Mwanza, Temeke na Zanzibar.
MANDAWA MCHEZAJI BORA WA VPL NOVEMBA
Mshambuliaji wa timu ya Kagera 
Sugar ya mkoani Kagera amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya 
Vodacom (VPL) kwa mwezi Novemba mwaka huu ambapo atazawadiwa kitita cha 
sh. milioni moja.
Mandawa ambaye kwa mwezi huo 
alichuana kwa karibu na mshambuliaji Fulgence Maganda wa Mgambo Shooting
 ya Tanga na nahodha wa Simba, Joseph Owino atakabidhiwa zawadi yake na 
wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya Vodacom.
Hafla ya kukabidhi zawadi hiyo 
inatarajiwa kufanyika wakati wa mechi ya raundi ya nane ya ligi hiyo 
kati ya Simba na Kagera Sugar itakayochezwa Desemba 26 mwaka huu kwenye 
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
KOZI YA UKUFUNZI WA UTAWALA YA FIFA SASA MACHI
Shirikisho la Kimataifa la Mpira 
wa Miguu (FIFA) limesogeza mbele kozi ya ukufunzi ya utawala wa mpira wa
 miguu iliyokuwa ifanyika Desemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa FIFA, kozi hiyo sasa itafanyika Machi mwakani katika tarehe itakayotangazwa baadaye.
TFF imepokea maombi ya zaidi ya 
washiriki 40 kwa ajili ya kozi hiyo itakayoshirikisha washiriki 30. 
Kutokana na maombi kuzidi idadi ya nafasi zilizopo, FIFA itafanya mchujo
 wa washiriki.

No comments:
Post a Comment