Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifuatana na Naibu Katibu Mkuu wa Chama
 Cha Mapinduzi Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai (wa kwanza kushoto) 
wakielekea kwenye ukumbi wa mkutano kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa 
semina ya uimarishaji Chama kwa mabalozi wa Lindi Mjini tarehe 
29.12.2014.
 Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai 
akifungua rasmi semina ya siku moja ya kuimarisha Chama kwa mabalozi wa 
Lindi Mjini tarehe 29.12.2014.
 Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai 
akifungua rasmi semina ya siku moja ya kuimarisha Chama kwa mabalozi wa 
Lindi Mjini tarehe 29.12.2014.
 Baadhi ya washiriki wa semina ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi kwa 
mabalozi wa Lindi Mjini wakifurahia hotuba ya mgeni rasmi Naibu Katibu 
Mkuu wa CCM Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai wakati akifungua semina hiyo 
huko Lindi tarehe 29.12.2014.
Mke
 wa Rais na Mjumbe wa NEC Taifa ya CCM Mama Salma Kikwete akiaagana na 
Mgeni Rasmi Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai 
aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe za ufunguzi rasmi wa semina ya siku
 moja ya mabalozi wa Lindi Mjini tarehe 29.12.2014.
Baadhi
 ya watoa mada (waliokaa mstari wa mbele) kwenye semina ya kuimarisha 
Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya mabalozi wa Lindi Mjini tarehe 
29.12.2014.
…………………………………………………………………………
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Matukio ya kutishia 
amani ya nchi na usalama wa raia yatapungua kama mabalozi wa nyumba kumi
 watafanya kazi zao kwa uaminifu kwani wao ni viongozi wa kwanza walio 
karibu na wananchi hivyo basi wanatakiwa kuwafahamu wakazi wa maeneo 
yao.
Hayo yamesemwa jana na 
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ally Vuai 
wakati akifungua semina ya siku moja ya  uwezeshaji wa chama hicho kwa  
mabalozi (viongozi wa mashina) wa wilaya ya Lindi mjini.
Vuai alisema Balozi ni 
kiongozi wa kwanza anayetakiwa kujua idadi ya wakazi wake, kazi 
wanazozifanya na majina yao kitendo ambacho kitasaidia kuimarisha 
usalama wa eneo husika lakini miaka ya hivi karibuni wameacha kufanya 
kazi hiyo kwa uadilifu na kuviachia vyombo vya dola pekee.
“Jukumu la kulinda amani
 ya nchi na usalama wa taifa letu ni la kila mtu, lakini hivi sasa kazi 
hiyo vimeachiwa vyombo vya dola pekee, mabalozi fanyeni kazi ya 
kuwatambua wakazi wa maeneo mnayoishi hii itasaidia kumtambua mualifu 
pale atakapofika katika eneo lenu”, alisema Vuai.
Alisema kikao cha kwanza
 cha CCM ni kikao cha shina hivyo basi mabalozi ni viongozi wa muhimu 
ndani ya shina wanatakiwa kutetea ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 na 
kutowaachia viongozi wakuu wa chama pekee kufanya kazi hiyo.
Vuai alisisitiza, “Muwe 
na uthubutu wa kujibu hoja potofu za wapinzani na kutokubali wawapotoshe
 wananchi juu ya mafanikio yaliyofanywa na Serikali. Kipindi 
cha uchaguzi kikifika endeleeni kuwahimiza na kuwasimamia wananchi 
wakapige kura ili wasipoteze haki yao ya msingi ya kupiga kura”.
Aliwataka mabalozi hao 
kuhakikisha wakati wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga 
kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika hapo mwakani 
wawahimize  wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi kujiandikisha 
majina yao.
Kwa upande wake Mjumbe 
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini 
Mama Salma Kikwete alisema mabalozi ni msingi na nguzo ya chama bila ya 
mabalozi chama hakiwezi kwenda vizuri ni kama vile binadamu anaweza kuwa
 na kila kitu lakini kama hana miguu hawezi kutembea.
Aliwapongeza kwa ushindi
 walioupata wakati wa uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za 
mitaa na kusema kuwa upendo na mshikamano ni msingi wa ushindi na usiri 
na uadilifu ni nyenzo muhimu katika utendaji wao wa kazi.
“Katika semina hii 
mtafundishwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kazi na wajibu wenu kwa
 Chama na Jamii inayowazunguka hivyo basi muwe wasikivu na kuyashika 
yale mtakayofundishwa na watoa mada”, alisisitiza Mama Kikwete.
Akiongea kwa niaba ya 
wajumbe walioshiriki semina hiyo Rashid Thabit kutoka kata ya Rahaleo 
alishukuru kwa mafunzo waliyoyapata na kusema kuwa yatawasaidia katika 
utendaji wao wa kazi.
“Tunakushukuru MNEC kwa 
ajili ya kuandaa mafunzo haya ambayo yametupa uelewa na wajibu na kazi 
zetu kama mabalozi. Uwepo wako wakati wa uchaguzi uliopita ulitufanya 
tukashinda kwani tulishiriki pamoja nawe katika kampeni za kuwanadi 
wagombea wetu”.
Nawaomba wajumbe 
wenzangu tusibweteke na ushindi huu bali tuongeze kasi na bidii na 
kuweza kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu utakaofanyika hapo mwakani 
ili tuweze kulikomboa jimbo la Lindi mjini kutoka mikononi mwa Chama Cha
 Wananchi (CUF)”, alisema Thabit.
Semina hiyo ya siku moja
 iliyohudhuriwa na wajumbe 993 kutoka kata zote 18 za wilaya hiyo 
iliandaliwa na Mama Kikwete ambaye aliwaahidi mabalozi kuwapa mafunzo 
hayo ili wajue majukumu yao ya kazi. Mada zilizojadiliwa ni kazi na 
wajibu wa mabalozi na katiba mpya iliyopendekezwa.







No comments:
Post a Comment