JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu 12 akiwemo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mshewe wakituhumiwa kwa kosa la kuua mtu kwa kumzika akiwa hai.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa lilitokea juzi majira ya saa 08:30 mchana novemba 6 mwaka huu katika kijiji cha Mshewe, kata ya Mshewe , tarafa ya bonde la Usongwe wilaya ya Mbeya vijijini Mkoani hapa.
Alimtaja marehemu kuwa ni Alison maarufu kwa jina la Hanahela Mwakabana(80) kyusa, mkulima, mkazi wa kijiji cha Mshewe ambaye aliuawa na kundi la wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi.
Alisema wauaji hao walikuwa wakiongozwa na Julius Katisha Ngole ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Mshewe baada ya kumfukia ndani ya kaburi akiwa hai.
Alisema chanzo cha mauaji hayo ni tuhuma za kishirikina baada ya marehemu kutuhumiwa kumuua mtoto wake Juma Hanahela(48) kyusa, fundi ushonaji, mkazi wa kijiji cha Mshewe aliyefariki dunia Novemba 5, mwaka huu kwa maradhi ya kiharusi ambayo alianza kuugua Oktoba 29, Mwaka huu na kulazwa hospitali teule ya Ifisi.
Kamanda Diwani alisema mbinu iliyotumika ni watuhumiwa baada ya kumaliza kuchimba kaburi walimwambia marehemu aingie ndani ya kaburi ili apime kama linatosha kumzika mtoto wake ndipo walipomfukia, kisha kuchimba kaburi lingine pembeni na kumzika mtoto wake Juma Hanahela.
Kwa mujibu wa Mjomba wa Marehemu ambaye alikuwa shuhuda wa tukio hilo,Edward Mwaikasu aliliambia JamboLeo kuwa wakati taratibu za mazishi ya mtoto wao zinaendelea aliwashauri kumwita mchungaji yeyote wa kanisa lililokaribu jambo ambalo liliafikiwa na Mwenyekiti wa Kitongoji.
Alisema wakati wakisubiri taratibu hizo kufanyika Mwenyekiti alisikika akimtuhumu Marehemu kuwa ndiye aliyemuua mwanae hivyo adhabu inayostahili dhidi yake inaandaliwa na lazima naye ashughulikiwe.
Alisema wakati Mwenyekiti akiongea hivyo waliokuwa wakichimba kaburi kwa ajili ya kumzika Marehemu walimwita wakitaka asaidie kuchimba shimo ambapowalimtaka kuingia ndani ya shimo na kutoa udongo ambapo baada ya kufanya hivyo walianza kumrushia udongo na kumfukia.
Alisema kutokana na tukio hilo Mwenyekiti alishauriwa apige simu polisi akidai kuwa Marehemu alifanya tukio msibani hivyo wananchi wenye hasira kali wamemuua hivyo nay eye kukubaliana na ushauri huo.
Kutokana na tukio hilo Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa kumi na mbili 12 kuhusiana na tukio hili wakiongozwa na Mwenyekiti Julius Katisha Ngole(52) msafwa, wote wakazi wa kijiji cha mshewe.
Kamanda Diwani alisema taratibu zinafanywa ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani na pia mwili wa marehemu ufukuliwe na kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ili uzikwe upya kwa heshima na taratibu zinazopaswa.
lakini mpaka hivi sasa mwili haujaweza fukuliwa na pia wananchi wametoweka kijijini hapo hivyo shughuli za kiuchumi kuzorota.
Picha na Shaaban Mpalule
|
No comments:
Post a Comment