Leo ni siku ya kupiga kura kwenye
Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji. Huu ni Uchaguzi Muhimu sana
katika nchi. Uchaguzi huu ndio MSINGI wa siasa kubwa za Kitaifa.
Siasa ya nchi inaanzia kwenye
Mtaa, Kijiji na Kitongoji. Na hakika, siku ya leo ilipaswa uwe ni
uchaguzi pia kwa ngazi ya Manispaa na Halmshauri, kwa maana ya
kuwachagua Madiwani.
Inahusu Serikali za Mitaa ( Local
Goverment). Nimepata kuandika, kuwa Mahtama Ghandhi alipata kusema, kuwa
ukitaka kuujua moyo wa nchi, nenda vijijini.
Katika nchi zetu hizi, uchaguzi wa
leo ni kipimo cha Uchaguzi Mkuu ujao. Chama ama kambi itakayofaulu
kupata asilimia 80 ya viti vyote vinavyogombaniwa, basi, naweza kuandika
hapa, Kuwa ni ndio chama au kambi itakayounda Serikali baada ya matokeo
ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwakani.
Na kama kwenda kupiga kura ni
kwenda kuchagua swali ni je, wapiga kura wanajua wanachokwenda kuchagua?
Jibu, yumkini kuna wapiga kura wenye kwenda kuchagua sura na majina ya
watu, lakini, kwa wengi waliohamasika au kuhamasishwa kujiandikisha, leo
Jumapili wanakwenda kuchagua wanachokijua na kukiamini.
Na siasa ni itikadi, na kwenye
itikadi, kama nilivyoandika huko nyuma, kuwa kuna KULIA na KUSHOTO. Ni
imani. Hivyo, kuwa na msimamo kisiasa ina maana ya kusimama ama Kulia,
au Kushoto. Kushoto ni wenye mrengo wa Kijamaa na Kujitegemea na kujali
zaidi maslahi ya walio wengi. Kushoto ni Mrengo wenye kusimamia katika
Haki na Usawa kwenye jamii. Kulia ni upande wa Mabwanyenye ama Mabepari.
Ni wenye kuamini zaidi katika Mtaji na kukuza mtaji, bila kujali
maslahi ya wengi. Na walio kwenye upande huo, wanaamini, kuwa Kutokuwepo
kwa Usawa kwenye jamii ni jambo lisiloepukika.
Na kuna Katikati ya kiitikadi,
kwamba kuna waliosimama kati. Lakini, aliyesimama kati anapo
anapoegemea. Hivyo, kuna waliosimama kati wakiegemea Kushoto na wengine
wakiegemea Kulia. Nao waweza kuwa viongozi bora, kama mpiga kura
atafanya maamuzi yake.
Leo tunakwenda kuwachagua viongozi
wetu kwenye Mitaa yetu, Vijiji na Vitongoji. Na kuna kisa cha mume
aliyegombea nafasi ya uongozi. Alikwenda kituo cha kupigia kura na
mkewe. Kura zilipohesabiwa aliambulia kura moja, ya kwake mwenyewe.
Nyumbani akamuulizia mkewe; ” Hivi mke wangu hata wewe hukunipigia
kura?”
Mkewe akajibu: ” Mume wangu,
tulikwenda kupiga kura kumchagua Kiongozi Bora, na kama ingelikuwa
kumchagua Mume Bora, kura yangu ingeangukia kwako!”
Naam, e twendeni tukapige kura kuwachagua viongozi bora, nao watokane na itikadi bora wenye kuzisimamia.
Ni Neno La Leo.
No comments:
Post a Comment