Na:Maryam Kidiko/Kijakazi Abdalla 
(Maelezo Zanzibar)
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya 
Muungano wa Tanzania Dk. Mohd Gharib Bilali amesema kuwa matumizi bora 
ya teknolojia ya habari yatawawezesha wanafunzi kupata elimu bora kwa 
urahisi.
Hayo ameyasema leo  katika skuli 
ya Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi Unguja wakati  wa uzinduzi wa darasa
 la kompyuta  ikiwa ni  miongoni mwa shamrashamra za kutimiza miaka 51 
ya Mapinduzi  ya Zanzibar.
Alisema kuwa matumizi bora ya 
kompyuta yatawafanya wanafunzi kuimarika vizuri kielimu wakati dunia  
hivi sasa imo katika mfumo  wa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ya 
habari.
Alisema kuwa teknolojia ya habari imekuwa kwa kiwango kikubwa jambo ambalo limekuwa likichangia ukuaji wa uchumi katika  Taifa
Amewashauri wanafunzi kutumia 
maendeleo ya teknolojia hiyo  kwa mambo yanayoweza kuwasaidia katika 
maendeleo ya masomo yao na maisha ya baadae.
“Vijana itumieni  teknolojia hii  katika njia zilizosahihi   ili iweze kuwaletea  faida” alisema Dkt. Bilali.  .
Amewataka wanafunzi  waongeze bidii  zaidi ili  waweza kumudu masomo hayo na kuleta maendeleo  katika jamii na nchi kwa ujumla .
Alisema kuwa matumizi ya komputa 
yanarahisisha kufundisha wanafunzi kwa njia rahisi na kuweza kujifunza 
mambo mbalimbali kupitia teknolojia hiyo na kupelekea kutanuka  kiakili.
Aidha Dkt. Bilali ameishukuru 
Serikali ya Jamhuri ya watu wa china kupitia kampuni ya ZTE kwa msaada 
wa kompyuta 50  na kuhakikisha kuwa teknolojia hiyo inaenea kwa kiasi 
kikubwa.  
Dkt. Bilali amesema msaada huo 
utaweza kuleta changamoto zaidi kwa wanafunzi na  kuwa  na wataalamu 
wengi waliobora kwa  maendeleo ya taifa Amesema  kuwa Serikali inathamini 
sana michango inayotolewa na marafiki wa maendeleo na Serikali 
itahakikisha michango hiyo inakuwa na faida kubwa kwa Taifa.
Katika risala  yao walimu wa skuli
 ya Kiembesamaki  wameiomba Serikali kuwawekea Uzio katika Eneo la skuli
 pamoja na usafiri kwa walimu na Wanafunzi.
Skuli  ya Kiembesamaki  Sekondari 
inajumla ya Wanafunzi 1,800 kwa sasa na katika sherehe za uzinduzi huo 
Dkt. Bilal amechangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya maendeleo ya 
skuli hiyo.

No comments:
Post a Comment