Kufuatia kukamilika kwa mchakato 
wa uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji na 
hivi sasa kuendelea kwa zoezi la kuapishwa kwa viongozi hao katika 
maeneo mbalimbali hapa nchini, kumejitokeza tabia ya baadhi ya wananchi 
kufanya vurugu na fujo katika zoezi hilo.
Baadhi ya wananchi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya 
kihalifu kwa kufanya fujo na vitendo vya vurugu ikiwemo kuwapiga baadhi 
ya watendaji wanaosimamia zoezi la kuapisha na kuwapiga viongozi wateule
 waliochaguliwa kihalali na wananchi kwa madai kuwa hawakushinda 
kihalali katika uchaguzi huo jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni 
na taratibu za nchi.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la 
Polisi nchini, linatoa onyo kwa wananchi wenye tabia hiyo kuacha mara 
moja na badala yake kama mtu hakuridhika na matokeo ya uchaguzi huo, 
afuate utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yake kwenye ngazi husika ili 
yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Jeshi la Polisi linawata Wakurugenzi na Maafisa watendaji
 wenye dhamana ya kusimamia mchakato wa kuwaapisha wenyeviti 
waliochaguliwa, kufuatilia kwa karibu migogoro inayojitokeza na kuitatua
 migogoro hiyo mapema ili kuepusha migongano inayoweza kusababisha 
uvunjifu wa amani.
Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu
 ama kikundi chochote kitakachofanya vurugu ama fujo kwa kisingizio cha 
ushabiki wa siasa na badala yake atakayebainika hatua kali za kisheria 
zitachukuliwa dhidi yake.
Imetolewa na:
Advera J. Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.

No comments:
Post a Comment