NA RAMADHANI ALI/MAELEZO ZANZIBAR
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar 
kupitia Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na 
watoto inaandaa zoezi la utambuzi wa wazee wenye umri  kuanzia miaka 60 
na kuendelea ili kutambua  sehemu wanazoishi na kuwaandalia mazingira 
mazuri ya maisha yao.
Akizungumza katika mkutano wa 
Kamati Tendaji ya Mpango huo katika Wizara ya Uwezeshaji Mwanakwerekwe, 
Mkuu wa kitengo cha Hifadhi ya Jamii Zanzibar Salum Rashid amesema zoezi
 hilo litafanywa  katika shehia zote za Zanzibar.
Amewaeleza wajumbe wa mkutano huo 
kwamba baada ya wazee hao kutambuliwa watapewa kadi maalum ambazo 
zitawasaidia kwenye huduma muhimu za msingi za kijamii zinazotolewa na 
Serikali  zikiwemo usafiri na matibabu bila malipo. 
“Lengo ni kuwaoredhesha wazee wote
 waliofikia umri kuanzia miaka 60  hapa Zanzibar kujua idadi yao 
kijinsia, Wilaya na Shehia zao na kuwapa vitambulisho  maalum 
vikavyowawezesha kupata huduma muhimu za kijamii bila malipo” 
alisisitiza Mkuu wa Kitengo cha Hifadhi ya Jamii.
Salum amesema maandalizi ya zoezi 
hilo yako katika hatua nzuri na litafanywa kwa uangalifu mkubwa ili 
 kuhakikisha kila aliefikia umri huo aweze kuoredheshwa kupitia shehia 
wanazoishi.
Katika kufanikisha mpango huo 
Wizara itaandaa vijana  wasiopungua 45 na kuwapa mafunzo  ya kazi hiyo  
na  kila shehia itakuwa na kijana mmoja ambae atashirikiana na  sheha 
ama mjumbe wake.
Amesema kwa mujibu wa sensa ya 
mwaka 2012 Zanzibar inaowazee 58311 wenye umri wa  kuanzia miaka 60  
ambao ni sawa na asilimia 4.5 ya wananchi wote.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa 
utafiti uliofanywa na  Shirika la HelpAge mwaka 2009, asilimia 60 ya  
wazee wenye umri huo hawana kipato rasmi cha kuendeleza maisha yao  na 
baadhi yao wamekuwa wakipata msaada mdogo kutoka kwa jamaa zao.
Amesema kutokana na usumbufu wa 
maisha unaowapata wazee hao ndipo Serikali ikaamua kuandaa mpango huo 
ili waweze kupatiwa msaada. 
Akizungumza katika mkutano huo 
Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, 
Wanawake na Watoto Msham Abdalla Khamis amesema  zoezi hilo halina 
uhusiano wowote na masuala ya siasa hivyo amewataka wananchi wasiwe na 
wasi wasi .
Amesema utaratibu kama huo wa  
kuwatunza na kuwasaidia wazee unafanyika katika nchi nyingi duniani na 
umekuwa na mafanikio makubwa kwao.
Aidha amesema lengo kuu la  mpango
 huo ni kuwatambua wazee sehemu wanazoishi  ili kuwasaidia  waweze 
kujikimu kimaisha na kuwapatia baadhi ya huduma muhimu za kijamii bila 
malipo

No comments:
Post a Comment