Mmoja wa wakazi kutoka katika Kata
 ya Nkoma iliyopo Wilayani Meatu mkoani Simiyu (kushoto) akitoa neno la 
shukrani mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo 
(kulia) baada ya Wizara ya Nishati na Madini kusambaza umeme katika kata
 hiyo kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili. Kijiji cha
 Nkoma ni moja ya vijiji 170 vilivyopo mkoani Simiyu vilivyofaidika na 
mradi wa umeme vijijini unaotekelezwa na REA Awamu ya Pili.
Waziri wa Nishati na Madini 
Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo katika moja ya mikutano 
aliyoifanya katika kata za Nkoma, Balyanaga, Kabondo na Bulyashi 
wilayani Meatu mkoani Simiyu.
Mtaalamu kutoka Kampuni ya LTL 
(PVT) LTD inayosambaza miundombinu ya umeme vijijini katika Wilaya ya 
Maswa chini ya mradi wa REA Awamu ya PIli Michael Marenye (kulia), 
akifafanua hatua iliyofikiwa ya uunganishaji wa umeme katika Kata ya 
Balyanaga mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo 
(kushoto) mara Waziri Muhongo alipofanya mkutano na wakazi wa Kata 
Balyanaga ili kusikiliza kero zao.
Sehemu ya wakazi wa Kata ya 
Mwambiti wakifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na Waziri wa
 Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) mara Waziri
 Muhongo alipofanya mkutano na wakazi hao.
Meneja wa Shirika la Umeme Nchini 
(Tanesco) Kanda ya Ziwa Mhandisi Joyce Ngahyoma akielezea namna ya 
kujiunga na huduma ya umeme mbele 
Na Greyson Mwase, Maswa.
Meneja Utaalamu Elekezi  kutoka  
Wakala wa Nishati  Vijijini (REA) Gissima Nyamohanga amesema kuwa 
serikali imetumia shilingi bilioni 881 katika mradi wa kusambaza umeme  
vijijini  unaotekelezwa na  Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya 
Pili.
Nyamohanga aliyasema hayo kwenye  
sherehe za uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini unaofadhiliwa na REA 
uliofanyika katika kata ya Shishiyu wilayani Maswa mkoani  Simiyu.
Alisema kuwa Mradi wa  REA  Awamu 
ya Pili  utaiwezesha  idadi ya  vijiji  vilivyounganishwa   na umeme 
3734  kati ya vijiji 15,180 ambayo ni asilimia 24.6 kufikia vijiji 5,234
 ambayo ni asilimia 34.5 ifikapo  mwezi Juni mwaka huu.
Aliongeza kuwa mradi wa REA Awamu 
ya Pili wa miaka miwili  ulioanza mwaka 2013, lengo lake lilikuwa  ni 
kuhakikisha kuwa vijiji vyote Tanzania vinapatiwa umeme hivyo kuboresha 
maisha  ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi.
Akielezea mchango wa mradi wa 
usambazaji wa umeme  vijijini  unaotekelezwa na  REA katika kuboresha 
maisha  ya wananchi Nyamohanga alisema kuwa awali wananchi  wote 
walikuwa wakilipa  shilingi  467,000 kama  gharama ya kuunganishiwa 
umeme ambayo ilikuwa ni kubwa na kupelekea  wananchi wachache wenye 
uwezo kuwa na  nishati ya  umeme huku  ikiacha kundi kubwa la wasio na 
uwezo kuishi  gizani.
Alisema kuwa katika Awamu ya 
Kwanza ya REA gharama za uunganishaji wa umeme  zilishuka kutoka  
shilingi 467,000 hadi shilingi 177,000 na kuongeza kuwa katika 
kuhakikisha  kila mwananchi anakuwa na uwezo wa kuunganishiwa umeme  
Serikali iliamua  kubeba  gharama zote kupitia REA Awamu ya Pili na 
wananchi kutakiwa kuchangia shilingi 27,000 tu kama kodi ya ongezeko 
(VAT)
Alieleza kuwa mara baada ya 
kumalizika  kwa Awamu ya Pili ya REA, viongozi wataainisha  vijiji 
ambavyo havijapata  umeme REA Awamu ya Pili, ambapo vitajumuishwa katika
 mradi wa REA Awamu ya Tatu.
Nyamohanga alieleza michango 
mingine kuwa ni  kufungua  fursa za ajira na uwekezaji kwa vijana wa 
kitanzania, ufaulu  kuongozeka kwa shule za sekondari na kuboreshwa kwa 
huduma za afya.
“Kwa mfano kwa shughuli za 
kiuchumi bei ya kusaga  debe la mahindi ilikuwa ni shilingi 1,000 
itashuka  hadi shilingi  500 kutokana na kwamba mashine za kusaga 
zitakuwa zinatumia  umeme badala ya  dizeli kama zamani,” alisema 
Nyamohanga
Wakati huohuo Meneja wa 
Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) Kanda ya  Ziwa Mhandisi  Joyce 
Ngahyoma akielezea jinsi ya kuunganishwa na huduma ya umeme kwa wananchi
 wa vijiji  vilivyopitiwa na mradi wa REA  Awamu ya Pili alisema kuwa 
wananchi wanaoishi  mita 30 karibu na miundombinu ya umeme 
wataunganishiwa kwa shilingi  27,000 na kuwataka kuchangamkia fursa hiyo
 kwa kuboresha makazi yao.
Alisema kwa wananchi wenye  nyumba
 zenye  vyumba viwili na vioski hawahitaji kufunga mfumo wa umeme kwenye
 nyumba zao (wiring) badala yake watashauriwa kununua kifaa maalumu 
kijulikanacho kama “UMETA” (Umeme Tayari) kinachoweza kutumika kama 
mfumo kwa kuwa na uwezo wa kuunganisha taa mbili na vifaa vingine  kama 
 vile jiko, friji na pasi.
Aliendelea kusema kuwa kifaa hicho
 kinachouzwa kwa gharama ya shilingi 37,000 kitakuwa ni mali ya mteja na
 endapo atahama makazi basi atakuwa huru kuhama pamoja na kifaa chake.





No comments:
Post a Comment