Kijana
 Musa Mchomvu akionyesha mfano wa andiko la mradi wa kikundi chake 
kijulikanacho kwa jina la Umoja ni Nguvu litakavyokuwa wakati wa semina 
ya uhamasishaji kwa vijana iliyotolewa na maafisa kutoka Wizara ya 
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
 leo Mkoani Kilimanjaro katika Wilaya ya Mwanga.
Vijana
 kutoka kikundi cha Tunza Mazingira wanaojishughulisha na upandaji wa 
miche ya miti Wilayani Mwanga wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Afisa 
vijana Bi. Amina Sanga (wapili kulia) walipotembelewa kwa ajili ya 
kuangalia maendeleo ya mradi wao. Kushoto ni Mwezeshaji wa Vijana kutoka
 Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Ester Riwa.
Maafisa
 kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na 
Wanakikundi cha Mwayo Net wakiangalia baadhi ya matofali yaliyofyatuliwa
 kwa kutumia mashine inayotumia udongo saruji wakati wa ziara ya 
kutembelea vikundi vya vijana Wilayani Mwanga.
Afisa
 Vijana Bi. Amina Sanga akiangalia moja ya mashine ya kufyatua matofali 
kwa kutumia udongo saruji walipotembelea kikundi cha Vijana cha Mwayo 
Net kinachojishughulisha na ufyatuaji wa matofali Mkoani Kilimanjaro 
katika Wilaya ya Mwanga.
Mwanakikundi
 wa kikundi cha Umoja ni Nguvu kinachojishughulisha na ufugaji wa Kondoo
 akitoa maelezo kuhusu kikundi chake walipotembelewa na maafisa kutoka 
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kukagua miradi ya Vijana 
wa Wilaya ya Mwanga. Katikati ni Afisa Vijana Bi. Amina Sanga na kulia 
ni Bw. John Masese.  
Mwezeshaji
 kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa 
akitoa maelekezo kuhusu uandikaji wa mradi wakati wa semina ya 
uhamasishaji kwa vijana kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana leo Mkoani 
Kilimanjaro katika Wilaya ya Mwanga.
………………………………………………………………..
Na: Genofeva Matemu – Maelezo
Tarehe: 09/01/2015
Vijana wa Mkoa wa Kilimanjaro wamewataka vijana wenzao kutokuwa 
na mtazamo hafifu unaowafanya kujenga fikra mbaya kati yao hivyo 
kushindwa kushirikiana katika kuendeleza mafanikio ya vijana katika mkoa
 wa Kilimanjaro.
Rai hiyo imetolewa leo na vijana walioshiriki semina 
inayoendeshwa na wawezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni 
na Michezo kuwaelimisha vijana kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, 
ujuzi pamoja na stadi za maisha.
Akizungumza wakati wa semina hiyo kijana Musa Mchomvu kutoka 
kikundi cha Umoja ni Nguvu amesema kuwa mtazamo wa vijana kuhusu Mfuko 
wa Maendeleo ya Vijana ulikua ni mdogo sana kutokana na vijana kutokuwa 
na elimu na uelewa wa kutosha hivyo kuwashukuru wawezeshaji waliotoa 
mafunzo juu ya mfuko huo na kuwataka vijana wazidi kushiriki semina 
zinazotolewa kwa vijana ili waweze kupata mwanga utakaowawezesha 
kujiendeleza.
Kwa upande wake Bibi. Salome Sichalwe amewataka vijana wa Mwanga
 kuweka siasa pembeni kwa kuachana na ahadi zinazotolewa na wanasiasa 
wanaowasababishia vijana kubweteka bali wajiwekee malengo 
yatakayowawezesha kuunda Saccoss imara ya Wilaya na kujiunga katika 
vikundi vya ujasiliamari kwa maendeleo ya Wilaya na Mkoa wa Kilimanjaro 
kwa ujumla.
Naye Bw. Idrisa Bajah wa kikundi cha Mwanga Youth Employment 
Fund amesema kuwa Wilaya ya Mwanga imekua na changamoto ya ajira kwa 
vijana lakini kutokana na semina waliyoipata itawasaidia vijana 
walioudhuria kuwanusuru vijana wenzao walioko mitaani kwa kuwapatia njia
 mbadala za kiujasiriamali.
Aidha mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na 
Michezo Bibi. Ester Riwa amesema kuwa vijana wengi wamekata tamaa 
kwasababu hawajitambui, hawatambui fursa zinazowazunguka na kukosa 
ubunifu kitu ambacho kinachowafanya kushindwa kutumia rasilimali ndogo 
zilizopo kujiendeleza.
Bibi. Riwa amezitaka Halmashauri kutekeleza mwongozo wa 
kuwasaidia vijana kupata mkopo unaotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya 
Vijana kwa kuunda Saccoss za Wilaya, kusimamia utengenezaji wa vikundi 
hai vya vijana na kuwaongoza vijana kuandika miradi iliyo na mashiko ili
 kufanikisha zoezi la kupatiwa mikopo inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo 
ya Vijana na kurejesha mikopo hiyo katika mfuko kwa ajili ya kupatiwa 
vijana wengine wanaohitaji mkopo
No comments:
Post a Comment